Kiwanda cha kuzalisha Sukari cha Bagamoyo (Bagamoyo Sugar),kinachomilikiwa na mwekezaji mzawa kampuni ya Bakharesa kinatarajia kuanza uzalishaji wake ifikapo Juni 2021.
Hayo yameelezwa na Meneja wa mradi huo Bw. Muharami Muharami, mapema wiki hii mara baada ya kamati ya Siasa ya Mkoa wa Pwani kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo unaotekelezwa katika kitongoji cha RAZABA kilichopo Kata ya Makurunge Wilayani Bagamoyo.
Mradi huo wa ujenzi wa kiwanda cha uzalishaji Sukari cha Bagamoyo Sugar upo katika hatua za awali za upandaji mbegu za miwa yaani “nursery” ambazo zimepandwa katika shamba lenye ukubwa wa hekta 8 ambazo zipo kwenye majaribio ya kutafuta mbegu moja bora itakayofaa kulimwa katika shamba hilo lenye ukubwa wa hekta 10,000 kwa kutumia mfumo wa kilimo cha umwagiliaji wa matone ujulikanao kama “drip irrigation”
Nae Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo akizungumza katika ziara ya ukaguzi wa mradi huo wa Shamba la miwa na ujenzi wa Kiwanda cha uzalishaji Sukari cha Bagamoyo Sugar amesema Serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe. Rais DK. John Joseph Pombe Magufuli katika kutekeleza Sera ya Tanzania ya Viwanda, ilitoa eneo hilo kwa kampuni ya Bagamoyo Sugar ambayo ni kampuni tanzu ya Bakhresa group of companies, iliyoomba kutekeleza mradi huo katika eneo hilo.
“Serikali baada ya kuchoshwa na uhaba wa sukari Nchini, iliamua kutoa eneo hilo kwa mwekezaji wa ndani, ili atekeleze mradi huo ambao uwekezaji wake utatumia jumla ya dola Milioni 75 na kiwanda hicho kipya cha sukari kinatarajia kuzalisha sukari kati ya tani 30,000 hadi 70,000 za sukari kwa Mwaka”Alisema Mhandisi Ndikilo
Akatumia fursa hiyo pia kuwahamasisha Wananchi wa eneo hilo na maeneo jirani kutumia fursa ya uwepo wa kiwanda hicho kulima miwa yaani “out growers” na kuuza kiwandani hapo mara uzalishaji utakapoanza ili waweze kunufaika na mradi huo na kujikwamua kiuchumi.
Katika hatua nyingine Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mhe. Ramadhan Maneno, amekemea tabia ya baadhi ya Wananchi kuvamia maeneo ya Wawekezaji na kuanzisha makazi ya kudumu na wengine kuingiza mifugo katika maeneo ya mashamba ya wawekezaji hali inayopelekea migongano isiyo ya lazima baina ya Wawekezaji na Wananchi.
Mhe. Maneno pia ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kwa kutekeleza miradi ya maendeleo yenye tija hususani mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Afya Kerege ambao umekamilika na umeanza kutoa huduma ambapo hadi sasa Wakina mama 127 wameshajifungua katika Kituo hicho kipya cha Afya.
Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Pwani ilifanya ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Mkoa Pwani ambapo wakiwa Wilayani ya Bagamoyo wametembelea jumla ya miradi sita ambayo ni pamoja na mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Kerege kilichopo Kata ya Kerege, Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo eneo la Mbegani, Ujenzi wa tanki la Maji lenye ujazo wa Lita Milioni sita (6) unaotekelezwa na DAWASA katika Kata ya Magomeni, mradi wa shamba la miwa na ujenzi wa Kiwanda cha Sukari cha Bagamoyo Sugar katika kitongoji cha RAZABA kilichopo Kata ya Makurunge, uzalishaji katika kiwanda cha Sayona kinachotengeza Juisi na kiwanda cha Vigae cha Twayford kilichopo Pingo chalinze.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.