Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa amesema kuwa Tanzania imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji wa miradi mbalimbali.
Mhe. Majaliwa aliyasema hayo alipotembelea kiwanda cha Bagamoyo Sugar Co. Ltd, kilichopo Makurunge Wilayani Bagamoyo kujionea utekelezaji wa mradi huo ambao Unatarajia kugharimu Dola za kimarekani milioni 100.
Akiwa katika eneo la mradi huo, Mhe. Majaliwa pamoja na kuzunguka kukagua namna utekelezaji wa mradi huo wa shamba la miwa na ujenzi wa kiwanda cha sukari unavyotekelezwa, amezugumzia jinsi Tanzania ilivyoweka mazingira mazuri ya uwekezaji hivyo kupelekea kupiga hatua kubwa katika sekta ya viwanda.
Mhe.Majaliwa ametanabahisha kuwa, Serikali ya Awamu ya tano iliamua kuinua uchumi wa ndani kwa kuimarisha uwekezaji wa sekta ya viwanda, ambapo matokeo yameshaanza kuonekana kwani sasa Nchi ya Tanzania imefikia uchumi wa kati kabla ya malengo iliyojiwekea kufikia ngazi hiyo ifikapo Mwaka 2025 na imetokana na maboresho makubwa ya mifumo ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa Sekta ya viwanda kwa kukaribisha wawekezaji wa ndani na wa nje.
“Maboresho haya makubwa ya mifumo yetu ya kiuchumi kupitia uwekezaji wa sekta ya viwanda yamefanikiwa kwakuwa Tanzania tumejitosheleza kuendesha sekta hii ya viwanda, tuna Amani inayofanya Tanzania kuwa mahali salama pa uwekezaji, tuna malighafi zinazotokana na ardhi nzuri tuliyonayo, wataalam wazoefu wa kutosha, miundo mbinu ya barabara, reli, maji na umeme ambayo inaendelea kuboreshwa kila uchao ambavyo vyote vinaifanya Tanzania kujitosheleza kiuwekezaji wa Sekta ya Viwanda” Amesema Mhe. Majaliwa.
Waziri Mkuu huyo ameongeza Kusekwa kuwa ili Sekta ya viwanda iendelee kufanya vizuri ni lazima eneo la malighafi liwekewe msisitizo. “Tunajua tuna malighafi za kilimo ambazo zinatumika viwandani, tuna malighafi za madini, maliasili na aina karibu zote za malighafi zinazotumika viwandani Tanzania zinapatikana, hivyo sisi Tanzania ni matajiri kwasababu hizi malighafi zote tunazo na tunaendelea kuwakaribisha wawekezaji wa ndani na wa nje kuja kuwekeza Tanzania kwani tunajitosheleza” Amesema Mhe. Majaliwa
Waziri Mkuu amefanya ziara maalum kutembelea kiwanda cha sukari cha Bagamoyo Sugar Company limited kilichopo eneo la Makurunge Wilayani Bagamoyo, kujionea uendelevu wa utekelezaji wa uwekezaji wa kiwanda hicho ambacho kinajengwa baada ya Serikali kuipatia Bakhresa group of companies eneo lenye ukubwa wa hekta 10,000 ili wafanye kilimo cha miwa na kujenga kiwanda cha sukari, uwekezaji utakaogharimu jumla ya Dola Milioni 100, huku Benki ya Wakulima Nchini (TADB) tayari ikiwa imeshatoa mkopo wa Dola Milioni 6.5 kusaidia uwekezaji huo, hivyo kuifanya Serikali kuwa mdau mkubwa katika uwekezaji huo ambao utaiondoa Tanzania katika upungufu wa takribani Tani 70,000 za sukari zinazohitajika kwa matumizi Nchini.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.