Serikali imetenga kiasi cha shilingi Bilion 40.1 kwa ajili ya ujenzi wa barabara zinazosimamiwa na TARURA Mkoani Pwani.
Hayo yamebainishwa Septemba 11, 2021 na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge mbele ya Kamati ya Siasa Mkoa iliyo Wilayani Mkuranga katika siku ya pili ya ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi- CCM Mkoani humo.
“Tayari tumepokea kiasi cha sh.bilion 1.1 za ujenzi wa barabara hizo ambazo ni pamoja na barabara ya Kiguza Mwanadilatu yenye urefu wa Kilomita 12.3 ambayo imetengewa sh. Milioni 139 na ujenzi wake unaendelea.” Amefafanua Kunenge.
Akizungumzia uboreshaji wa miundombinu ya barabara za vijijini, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Pwani Ramadhani Maneno amewaondoa hofu wananchi kuhusiana na barabara hizo na hasa zinazohitaji marekebisho kwamba Serikali imeziweka kwenye mpango wa matengenezo.
Mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Hoyoyo Hafija Dengwa amesema ujenzi wa barabara ya Kiguza-Mwanadilatu utaondoa kero iliyokuwa inawakabili ya kukatika mawasiliano hasa kipindi cha mvua.
Naye Hassan Luhongo mkazi wa Hoyoyo alisema barabara hiyo ikikamilika itapunguza msongamano kwa barabara ya Mbagala jijini Dar es salam.
Hassan amesema Serikali ikikamilisha ujenzi wa barabara hiyo wananchi wanaoenda Chanika, Kisarawe na Kibaha watapata urahisi badala ya hali iliyopo sasa ambapo wanazunguka Mbagala eneo ambalo linaelezwa kuwa na msongano wa magari.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.