Mkuu wa Mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo amewataka walengwa wanaoendelea kupokea ruzuku ya fedha toka mfuko wa maendelea ya jamii TASAF kuhakikisha wanazitumia fedha hizo vizuri kwa kujiwekea malengo maalum ya kimaendeleo .pamoja na kujiwekea akiba
Rai hiyo ameitoa wakati alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya ajira za muda zinazotekelezwa na walengwa wa TASAF Wilayani Bagamoyo ambapo alitembelea mradi wa upandaji wa Miti ya Mikoko pembezoni mwa Pwani ya bahari ya Hindi katika Kijiji cha Kondo kilichopo Kata ya Zinga na mradi wa Ujenzi wa Lambo uliopo katika Kijiji cha Rupungwi Kata ya Mandera.
“Ni rai yangu kwa walengwa wanaoendelea kupokea ruzuku hii ya fedha toka mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF kuhakikisha wanazitumia fedha hizo vizuri kwa kujiwekea malengo maalum ya kimaendeleo na kuyatimiza ikiwemo kuboresha makazi yenu kwa kujenga nyumba bora, niwakumbushe kuweka akiba lakini pia kuwekeza katika kufungua miradi endelevu ili mpango utakapofikia tamati msirudi katika umasikini mliokuwa nao awali bali msonge mbele mkiwa tayari na uwezo wa kujitegemea kiuchumi anaongeza” Alisema Mhandisi Ndikilo.
Aidha aliendelea kusema kuwa, TASAF imekua mkombozi kwa Wananchi masikini katika Mkoa wa Pwani ambapo umewezesha baadhi ya familia kupata milo mitatu kwa siku, kuanzisha miradi midogo midogo ya biashara na hivyo kujijengea uwezo wa kujitegemea kiuchumi, kuboresha mahudhurio ya wanafunzi mashuleni na kwa watoto walio chini ya miaka mitano wanaotimiza masharti ya afya nao pia mahudhurio yao kliniki yameboreka anasema na Wananchi wameweza kukata bima ya afya kupitia mfuko wa Afya ya jamii CHF, bima inayowasaidia kujipatia uhakika wa matibabu wao na familia zao.
Akiwa katika Kijiji cha Rupungwi, Mhandisi Evarist Ndikilo, pia alipata nafasi ya kushiriki zoezi la ugawaji fedha za ruzuku kwa Walengwa 75 wanaopatikana katika Kijiji hicho na kutumia fursa hiyo kuongea na Wananchi wa Kata ya Mandera akiwahimiza juu ya kuacha vitendo vya uhalifu kila mmoja kuwa mlinzi wa Mwenzake, kushiriki katika shughuli za ulinzi shirikishi ili kuhakikisha eneo hilo halitajwi katika vitendo vya kihalifu vya kuvamia magari na kupora maduka kwa magobore kama ilivyo sasa.
Katika Hatua nyingine Mhandisi Evarist Ndikilo ameupongeza mpango wa ajira za muda kwa walengwa wa TASAF Wilayani Bagamoyo, unaotekelezwa na mfuko wa maendeleo ya jamii TASAF.
Mpango wa ajira ya muda kwa walengwa wa mpango wa TASAF Wilayani Bagamoyo ilianza utekelezaji wake Mwaka 2015 ambapo katika mwaka wa fedha 2015/2016 jumla ya Tshs.1,292,761,000.00 zililipwa kwa Kaya za walengwa 10,363, Wanawake wakiwa 8,614 na Wanaume 1,749 huku miradi 14 ikiibuliwa na kutekelezwa na Walengwa na kwa Mwaka 2016/2017 miradi 98 iliibuliwa, ambapo Kaya 9,265 zilishiriki kufanya kazi za ajira kwa muda na kulipwa kiasi cha 1,215,064,700.00 na kwa Mwaka 2017/2018 jumla ya miradi 103 iliibuliwa na kutekelezwa ambapo jumla ya Kaya 8,330 zimeshiriki kufanya kazi za ajira kwa muda na kulipwa Tshs. 723,856,000.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.