Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imetoa kiasi cha Sh. milioni 20 kwa ajili ya kusaidia kutatua Changamoto za wahanga wa mafuriko yaliyotokea katika Wilaya ya Kibiti na Rufiji Mkoani Pwani.
Mfano wa hundi ya fedha hizo imekabidhiwa leo na meneja mahusiano wa TFS nchini Johary Kachwamba kwa mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge katika hafla iliyofanyika ofisi za Mkuu huyo zilizopo Mjini Kibaha.
Kachwamba, amesema kuwa TFS kupitia Kamishna wake Silayo Dos Santos imeguswa na janga hilo la mafuriko ndio maana imeona kuna kila sababu ya kuunga mkono Serikali kwa kusaidia wahanga wa Wilaya hizo.
Amesema kuwa TFS kwa eneo la Rufiji wanamisitu na kwamba wana - Rufiji ni wahifadhi wenzao kwa kuwa TFS ina misitu zaidi ya 10 ikiwa na zaidi ya hekta 32,000 ndio maana Kamishna wa Uhifadhi ameridhia kutoa kiasi hicho ili kusaidia wahanga hao.
Amesema kuwa pamoja na kutoa mchango huo, bado TFS itaendelea kuwashika mkono katika kutatua changamoto mbalimbali pale ambapo itahitajika kwa kuwa jambo hilo linahitaji ushirikiano wa pamoja.
"TFS kupitia Kamishna wa Uhifadhi Silayo Dos Santos imetoa kiasi cha Sh. milioni 20 kusaidia changamoto za wahanga wa mafuriko Rufiji na Kibiti lakini tutaendelea kushika mkono kulingana na mahitaji ," amesema Kachwamba.
Akizungumza mara baada ya kupokea hundi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge ameishukuru TFS kwa mchango huo kwani wameonyesha namna ambavyo wameguswa na janga la mafuriko hayo.
Kunenge, amesema kuwa TFS wamefanya jambo hilo kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kwamba kitendo hicho kinampa faraja Rais katika kuwatumikia Wananchi.
"Nawashukuru sana wenzetu wa TFS kwa kutoa mchango huu mkubwa kwa ajili ya kusaidia wahanga wa mafuriko Wilayani Kibiti na Rufiji, ni mfano wa kuigwa kwao kwakuwa wanaunga mkono Rais Samia," amesema Kunenge.
Mkuu huyo wa mkoa amesema kuwa pamoja na kutoa mchango wa fedha hizo, TFS wameonesha moyo wa pekee kwani kabla ya kutoa fedha hizo tayari wametoa eneo na viwanja kwa ajili ya kufanyia shughuli za mafuriko.
Pia ameahidi kuzitumia fedha hizo katika kutoa huduma kwa wahanga wa mafuriko hayo huku akiwaomba TFS kuendelea kumuunga mkono Rais Samia na kuhakikisha wanatoka katika kutumia nishati ya mkaa na kwenda katika nishati mbadala.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.