Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ameutaka uongozi wa kiwanda cha Biotech Tanzania kinachotengeneza dawa ya kuulia viuadudu pamoja na bodi ya NDC, kutumia vyombo vya habari katika kuitangaza dawa inayozalishwa katika kiwanda hicho.
Hayo ameyasema wakati wa ziara yake ya ukaguzi aliyoifanya katika kiwanda hicho cha Biotech kilichopo Mjini Kibaha Mkoani Pwani.
“Katika ukaguzi nilioufanya bado nimekuta kuna lundo la dawa ambayo haijapata soko, hivyo nauagiza uongozi wa kiwanda hiki pamoja na bodi ya NDC kutumia vyombo vya habari kuitangaza dawa inayozalishwa katika kiwanda hiki ili wananchi wajue”alisema mhe. Majaliwa
Akiwa kiwanda hapo Mhe. Majaliwa alisema kuwa amefarijika kukuta uwekezaji mkubwa katika kiwanda hicho ikiwa ni utekelezaji wa sera ya Serikali ya awamu ya tano na kuongeza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha inashirikiana na mataifa rafiki ikiwemo Cuba katika kuhakikisha wanawekeza hapa nchini.
Mhe. Majaliwa aliendelea kusema kuwa kiwanda hicho ni kikubwa Barani Afrika na ujenzi wake ulitokana na mkopo kutoka Serikali ya Cuba.
Aidha ametoa wito kwa taasisi mbalimbali na wananchi kufika kiwandani hapo na kununua dawa hiyo kwa ajili ya kuulia mazalia ya Mbu wakiwemo mbu waenezao ugonjwa wa Malaria .
Katika Hatua nyingine Mhe. Majaliwa ameiagiza Mikoa yote Tanzania Bara iendelee na kampeni za kutokomeza malaria kwa kuwahamasisha wananchi kuweza kununua na kutumia dawa hiyo ya kuulia viuadudu..
Nae Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo alisema kuwa Mkoa tayari ulishafanya uhamasishaji wa ununuzi na utumiaji wa dawa kwa jamii ambapo katika kampeni hiyo wafanyabiashara wa Mkoa wa Pwani walichangia lita 300 ambapo dawa hizo ziligawanywa kwa wananchi bure siku ya uhamasishaji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.