Hali ya matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka huu Mkoani Pwani, imepanda kutoka asilimia 62.57 mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 66.9 mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 4.33 .
Pamoja na kupanda kwa ufaulu bado Mkoa huo haujafikia kiwango cha ufaulu kitaifa ambacho ni asilimia 72.4 hivyo Mkoa umeshika nafasi ya 19 kitaifa ambapo mwaka Jana ulishika nafasi ya 21.
Kutokana na hali hiyo imefanya Mkoa wa Pwani kuwa kati ya mikoa kumi iliyoongeza ufaulu kitaifa.
Akitoa taarifa hiyo kwenye kikao cha bodi cha matokeo ya wanafunzi kujiunga kidato cha kwanza mwaka 2018, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Elimu Bw. Abdul Maulid, alieleza kuwa wanafunzi waliofanya mtihani walikuwa ni 27,268 ambapo wanafunzi 18,242 sawa na asilimia 66.9 walifaulu.
Alisema wanafunzi hao waliohitimu darasa la saba walipata alama 100-250 kati yao 379 walipata daraja A huku wanafunzi 4,251 wakipata daraja B na wanafunzi 13,612 daraja C na wote hao wataendelea na elimu ya sekondari.
Maulid alisema, wanafunzi 101 sawa na asilimia 0.37 hawakufanya mtihani kwasababu mbalimbali ikiwemo mimba wanafunzi 20, wanafunzi wengine 60 ni watoro, vifo 6 , ugonjwa 12 na sababu nyingine wanafunzi watatu.
Aidha ameeleza kuwa, bado ipo changamoto katika kukabiliana na tatizo kubwa la utoro hivyo juhudi za pamoja zinahitajika ili kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi wa kudumu .
Maulid alitaja shule za msingi zilizofanya vizuri kimkoa ni Carissa, Marian, Lifewaylight, St.Antony, White Angels, New Version, Chalinze Modern, Philadelphia, Stone Of Help na Mwasama iliyopo Dunda Bagamoyo.
“Shule zilizofanya vibaya ni Vunduma ya Talawanda-Chalinze, Pera-Chalinze, Nyamato-Mkuranga, Kifuleta-Chalinze, Koma-Mkuranga, Kivinja B -Kibiti, Nyamakurukuru-Rufiji, Mkenda-Kibiti, Kwakonje-Chalinze na Mbuchi-Kibiti” alitaja Maulid.
Maulid alibainisha kati ya Halmashauri zilizopo Mkoani Pwani, Halmashauri ya Mji wa Kibaha imeongoza kwa kuwa na asilimia 80.92 kutoka 76.28 kipindi kilichopita.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bw. Zuberi Samataba alisema, kila Halmashauri inawajibu wa kutafuta sababu zilizopelekea kufanya vibaya kwa shule hizo kumi ili kupata ufumbuzi wa haraka.
Alieleza Serikali iliweka wastani wa asilimia 80 ya ufaulu kwa shule za msingi ikiwa ni mkakati wa kufikia mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN).
Samataba alisema kufuatia mkakati huo kuna kila sababu ya wadau wa elimu kupiga vita utoro na mimba za utotoni ili hali kufikia mkakati huo.
Aliwataka walimu, wazazi kushirikiana na Idara ya Elimu Wilaya na Mkoa kukabiliana na changamoto zinazosababisha taaluma kushuka ili kuhakikisha matokeo ya mwaka ujao yanapanda zaidi ya sasa.
Akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo aliliagiza Jeshi la Polisi Mkoa kuwasaka wale wote waliohusika kuwapa mimba wanafunzi 20 na kusababisha kushindwa kufanya mtihani wao wa mwisho.
Alisema, wanaume wanaowatongoza watoto wa shule, wanatakiwa kushtakiwa kwa mujibu wa sheria na kufungwa miaka 30 jela.
Mhandisi Ndikilo, alibainisha kuwa ufaulu kwa mwaka huu umeweza kupanda na kufikia asilimia 66.9, ni hatua nzuri na aliwapongeza walimu ,viongozi wa ngazi zote na jamii.
Pamoja na hayo alisema ufaulu umeongezeka katika Halmashauri ikiwa ni sanjali na Kibiti 54.02 na Rufiji 52.94 licha ya wilaya hizo kukumbwa na hali ya kiuhalifu kwenye kipindi hicho
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.