Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amewataka viongozi wa taasisi za umma na binafsi kuwa mabalozi wa ulipaji kodi na kuhakikisha watumishi walio chini yao wanadai risiti kila wanapofanya manunuzi, akisisitiza kuwa ukwepaji wa kodi unadhoofisha uchumi wa nchi.
RC Kunenge ametoa kauli hiyo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Mlipa Kodi yaliyofanyika Kibaha, mkoani Pwani, ambapo aliipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa juhudi zake za kuthamini na kuwashukuru walipakodi wanaotekeleza wajibu wao kwa uaminifu.
Amesema ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha analipa kodi stahiki kwa hiari, kwani kodi hizo ndizo zinazoiwezesha serikali kutoa huduma muhimu kama elimu, afya, miundombinu, na usalama.
RC Kunenge ameonya kuwa ukwepaji wa kodi ni hatari kwa uchumi wa taifa, kwani unapunguza mapato ya serikali na kudhoofisha uwezo wake wa kutoa huduma kwa wananchi. Ameeleza kuwa kuna tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kushusha bei za bidhaa na huduma ili wasitoe risiti sahihi kwa wateja, hali inayosababisha upotevu mkubwa wa mapato ya serikali.
Amepongeza walipakodi waliotunukiwa tuzo kwa kutimiza wajibu wao ipasavyo na amewahimiza kutumia zawadi hizo kama motisha kwao na kwa wengine ili kuongeza uaminifu katika ulipaji kodi.
Kwa upande wake, Meneja wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Bw. Richard Kayombo, amesema kuwa vigezo vilivyotumika kuwapata walipakodi bora ni pamoja na ulipaji kodi kwa hiari, matumizi sahihi ya mashine za EFD na stempu, pamoja na mchango mkubwa wa kodi kwa serikali.
Naye Meneja wa TRA Mkoa wa Pwani, Bw. Masawa Masatu, amesema mamlaka hiyo inatambua mchango wa walipakodi katika kukusanya mapato yanayowezesha serikali kuboresha sekta mbalimbali kama afya, ulinzi, na huduma nyingine muhimu.
Ameeleza kuwa changamoto kubwa inayoathiri makusanyo ya kodi ni ukosefu wa uaminifu kwa baadhi ya wafanyabiashara, ambao huwashawishi wateja kwa kushusha bei ili wasitoe risiti za kielektroniki (EFD) zenye thamani halisi ya bidhaa au huduma.
RC Kunenge amewataka wananchi wote kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha kodi inalipwa kwa uaminifu, akisema kuwa kulipa kodi ni uzalendo na ndio msingi wa maendeleo ya taifa. Amewahimiza wananchi kudai risiti kila wanapofanya manunuzi na kuripoti wafanyabiashara wanaokwepa kodi ili kudhibiti upotevu wa mapato.
Uchumi imara wa taifa letu unategemea ulipaji wa kodi. Ukwepaji kodi ni hujuma kwa maendeleo ya nchi na unadhoofisha juhudi za serikali za kuboresha huduma kwa wananchi. Hivyo, tushirikiane kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake,amesema RC Kunenge.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.