Jumla ya vituo 3,941 vya kupigia kura vimeandaliwa katika Mkoa wa Pwani kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, ikiwa ni juhudi za Serikali kusogeza huduma hiyo karibu zaidi na wananchi na kuhakikisha kila mmoja anapata nafasi ya kutekeleza haki yake ya kikatiba.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Mhe.Abubakar Kunenge, alisema maandalizi yote muhimu yamekamilika kwa kiwango cha kuridhisha, na vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea wakati wa uchaguzi.
“Kamati ya usalama imeweka mikakati madhubuti na ina taarifa za kina kuhusu hali ya kila eneo la mkoa. Wananchi wasiwe na wasiwasi, wajitokeze kwa utulivu kwenda kupiga kura siku ya uchaguzi,” alisema Kunenge.
Ameongeza kuwa serikali imeendesha programu za elimu kwa umma na makundi mbalimbali kuhusu umuhimu wa kushiriki katika uchaguzi kwa amani, utulivu na uwajibikaji wa kiraia.
“Nawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi kupiga kura. Waende wakachague viongozi watakaoweza kutatua changamoto zenu na kuwaletea maendeleo, kulingana na sera zilizowasilishwa na vyama vyao,” alisisitiza.
Aidha, Kunenge alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutangaza siku ya uchaguzi kuwa mapumziko rasmi ya kitaifa, hatua itakayowawezesha wananchi wote kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo muhimu.
Kwa mujibu wa Kunenge, vituo vya kupigia kura vitafunguliwa kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni, na wapiga kura watakaokuwa bado kwenye foleni muda wa kufunga vituo utakapowadia, wataruhusiwa kupiga kura hadi wote watakapomaliza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.