Tanzania imeanza kuzalisha dawa ya kwanza ya kibaolojia kwa ajili ya kuua wadudu waharibifu wanaoshambulia mimea na mazao ya kilimo.
Kauli hiyo imetolewa leo septemba 21, 2023 na Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Ashantu kwenye kikao na waandishi wa habari kilichofanyika katika kiwanda hicho kilichopo Halmshauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani.
Ameelza kuwa dawa hiyo ni bidhaa ya pili ya viuatilifu hai ambayo inazalishwa na kiwanda cha BIOTECH ambacho pia kinazalisha Viuatilifu vya kuua viluwiluwi vya mbu.
“Tayari dawa hii imepata ithibati, imesajiliwa na Wizara ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Afya za Mimea na Viuatilifu, hivyo nataka Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Taifa la NDC kusimamia kiwanda hiki ili kuhakikisha dawa hizo zinazalishwa kwa wingi na kuingizwa sokoni ifikapo mwezi Oktoba zianze kutumika katika msimu ujao wa kilimo," amesema Dkt. Kijaji.
Aidha, amesema tayari amefanya mazungumzo na Waziri wa Kilimo ili dawa hizo zianze kupatikana katika maduka yote ya pembejeo za kilimo nchini ili kuwawezesha wakulima kupata mazao mengi shambani.
Nae Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Maendeleo la Taifa NDC, Dkt. Nicolaus Shombe amesema wamepokea maelekezo hayo na kwamba utekelezaji wake unaanza mara moja.
Dkt. Shombe amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha viuatilifu vya kuua viluwiluwi vya mbu lita milioni sita za dawa kwa mwaka lakini kwa sasa wanazalisha dawa lita milioni moja hivyo wataongeza kasi ya kuzalisha dawa za kuua mbu lakini pia dawa za kuua wadudu wanaoshambulia mimea.
Kwa mujibu wa Waziri Dkt. Kijaji, Tanzania iliingia mktaba wa eneo huru la biashara barani Afrika kwa ajili ya kuuza bidhaa zake nje ya nchi na kwamba tayari wamefikia nchi saba kuuza bidhaa zake lakini pia tayari imeingiza bidhaa nne na hivyo kuanza kuzalishwa kwa bidhaa hiyo itaifanya Tanzania kuwa na bidhaa tano zinazouzwa ukanda wa Afrika
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.