Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani Zuwena Omari amewaasa waandishi wa habari kutumia nguvu ya kalamu zao kuandika taarifa za mradi wa Shule Bora unaolenga kuweka mikakati sahihi na kutafuta suluhisho ili kuhakikisha Watoto wa makundi maalum, wa kike na wa kiume wanapata elimu iliyo kwenye mazingira bora.
Rai hiyo ameitoa leo Disemba 8, 2022 wakati akifungua mafunzo ya uhamasishaji wa mradi wa Shule Bora kwa waandishi wa habari na wasimamizi wa vyombo vya habari mkoani humo ambapo pia aliwaasa kuendelea kuimarisha mahusiano baina ya Serikali na vyombo vya habari ili mradi huo ulete tija.
"Hakuna asiyejua nguvu ya kalamu za waandishi wa habari, kwa kuandika taarifa zinazoaminika kwenye kampeni za maendeleo nchini, sisi Kama mkoa tutaimarisha mahusiano na vyombo vya habari ili kuhakikisha mradi unaleta mafanikio "alifafanua Zuwena.
Akielezea mradi huo, Zuwena alibainisha kuwa umefadhiliwa na mfuko wa UKaid unaolenga kuunga mkono uboreshaji wa elimu msingi Tanzania kwa miaka sita katika Halmashauri 67 mikoa 9 yaTanga, Pwani, Dodoma, Singida, Kigoma, Katavi ,Simiyu, Mara na Rukwa na itahusisha watoto milioni 3.8 katika maeneo hayo ya utekelezaji.
"Utekelezaji wa mradi umelenga kuboresha ufundishaji kwa walimu, kuboresha elimu awali na ya msingi iliyo jumuishi kwa makundi ya watoto wenye mahitaji maalum, kuboresha ujifunzaji kwa wanafunzi pamoja na kuboresha mfumo wa usimamizi wa sekta ya elimu katika kuhakikisha kila kiongozi anawajibika ipasavyo kwa nafasi yake ili kufikia azma iliyokusudiwa" alisema Katibu Tawala huyo.
Kwa upande wake Afisa elimu mkoa wa Pwani Sara Mlaki alieleza kuwa mradi wa Shule Bora ulizinduliwa Kitaifa na Kimataifa mwaka 2021 katika shule ya msingi Mkoani kwenye Halmashauri ya Kibaha Mji mkoani Pwani.
Sara lifafanua kuwa kwa sasa zipo kazi zinazoendelea kufanywa kulingana na matakwa ya mradi ikiwa ni sanjari na uboreshaji wa aufundishaji darasa madarasa ya awali, uimarisha usimamizi wa shule na elimu katika Mamlaka za Serikali za mitaa ambapo wameshaanza kuona matokeo chanya kwani ufaulu umepanda.
Sara alieleza mradi huo unakusudia kuondoa changamoto zinazowakabili watoto kushindwa kusoma, kuandika na kuhesabu, kuondoa tatizo la utoro na kutowapa fursa watoto wenye mahitaji maalumu katika kuendelea na elimu ya sekondari.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa habari Mkoani Pwani, Ally Hengo alishukuru kundi la waandishi kutambuliwa na kushirikishwa kwenye utekelezaji wa mradi huo na akaeleza kuwa wanashukuru waandishi kuachiwa mlango wazi kupata taarifa ama kupewa ufafanuzi juu ya masuala ya elimu kupitia maafisa habari kwani changamoto kubwa wanayoipata ni kukosa taarifa kwa wakati.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.