Watumishi mbalimbali kutoka Mkoni wa Pwani wameungana kwa pamoja na kufanya maandamano ya amani yaliyolenga kumpongeza Mhe. Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli, kwa kuweza kurejesha kikokotoo cha zamani cha mafao ya Wastaafu.
Maandamano hayo yamefanyika mwishoni mwa wiki hii katika viwanja vya Shirika la elimu Kibaha, ambapo yalijumuisha wafanyakazi wote wa Serikali , mashirika ya umma pamoja na Sekta binafsi, maandamano hayo yalipokelwa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo, ambaye ndie alikuwa mgeni rasmi.
Akisoma hotuna kwa niaba ya wafanyakazi , mratibu wa Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi [TUCTA] Mkoa wa Pwani , Kassim Matewele alisema pamoja na nia njema ya Serikali ya kuunganisha mifuko hiyo ya jamii yapo mambo ambayo wanachama wa mifuko hiyo hawakuridhishwa nayo, ikiwa pamoja na {fomula} yaani kikokotoo kilichotumika ambacho kilipunguza mafao ya watumishi kwa asilimia 62.9%.
Aidha Matewele alisema kuwa Wafanyakazi wamepokea kwa furaha na wamekuwa na faraja kubwa na maamuzi ya Mhe. Rais na kusema kuwa uamuzi huu ni wa kiungwana na umeonesha kuwajali wafanyazi hasa wastaafu waliotumikiaTaifa hili.
“ Tunampongeza Mhe. Rais Magufuli kwa kuamua kurudisha kikokotoo kilichokuwa kikitumika awali kwa mifuko yote.Kupitia maandamano haya sisi wafanyakazi wa Mkoa wa Pwani tunampongeza na tunamshukuru sana Mhe. Rais kwa uamuzi wake wa busara kwa kujali maslahi ya wafanyakazi na Taifa kwa ujumla.
Matewele aliendelea kusema kuwa pamoja na uamuzi huo wa Serikali, pia wanayo maombi kadhaa kwa Mhe. Rais ikiwa ni pamoja na kuomba kupandishiwa mishahara, madaraja , vyeo na ulipaji wa malimbikio pamoja na urekebishaji wa mafao kwa baadhi ya mifuko ya jamii kama GEPF, PPF, NSSF ambapo wameomba mifuko hiyo wapandishe nao wafike asilimia 50%.
Akionge a mara baada ya kupokea hotuna ya wafanyakazi , Mkuu wa Mkoa wa Pwani , Mhandisi Evarist Ndikilo nae ameungana na wafanyakazi hao katika kumpongeza Mhe Rais kwa namna alivyotolea Tamko suala hilo.
Mhandisi Ndikilo alisema kuwa alichokifanya Mhe. Rais ni jambo kubwa na la neema na heshima kwa wafanyakazi.
“ Serikali ya awamu ya Tano chini ya Uongozi wa Mhe. Rais Dkt John Pombe Magufuli ni sikivu sana na inawajali wanyonge na inachukua hatua stahiki kwa wakati na muda muafaka alisema Mhandisi Ndikilo.
Aidha amewataka watumishi wote kwenda kufanya kazi kama kauli mbiu ya hapa kazi tu inavyohamasisha.
“Kila mtu kwa kwa nafasi yake aende akawajibike, na sisi Serikali tunahidi kuendelea kutimiza wajibu wetu kama ambavyo mmetupa dhamana ya kuwaongoza “ alibainisha Mhandisi Ndikilo.
Sambamba na hilo Mhandisi Ndikilo amewapongeza watumiashi wa Mkoa wa Pwani kwa kuwa na nidhamu katika kazi ambapo wamekuwa wakiwahudumia wananchi vizuri na kuondoa malalmiko kwa wananchi.
Katika Hatua nyingine Mhandisi Ndikilo amekemea vikali vitendo vinavyofanywa na wamiliki na waajiri wa viwanda wanaowafanyisha watumishi wao kazi katika mazingira magumu na hatarishi.
“Sasa natoa onyo kwa wamiliki na waajiri wa viwanda kuwa Viwanda tunavitaka ila tunahitaji staha kwa watumishi , hivyo basi tutachukua hatua kali kwa mmiliki yeyote atakaenda kinyume na hili hatutamvumilia kwa lolote “ alisema Mhandisi Ndikilo.
Nae kwa upande wake Mwenyekiti wa TUCTA Mkoa Pwani alisema kuwa vyama vya wafanyakazi vitaendelea kutumia njia ya majadiliano na Serikali katika kutatua au kumaliza matatizo yote yanayowakabili wafanyakazi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.