Wajumbe wa bodi ya Barabara ya Mkoa wa Pwani imetaka kupitiwa upya kwa mkataba wa mkandarasi wa barabara ya Tamco Kibaha kwenda Mapinga wilayani Bagamoyo wa kampuni ya Skol kutokana na kusuasua kuanza ujenzi wa sehemu ya barabara hiyo.
Wakizungumza kwenye kikao cha bodi ya barabara ya mkoa huo baadhi ya wajumbe walisema kuwa wanashangaa kuona mkandarasi huyo tangu apewe kazi hakuna alichokifanya hivyo kuona kuwa kuna haja ya kuangaliwa upya kwa mkataba wake.
Akizungumza kwenye kikao hicho mkuu wa mkoa Mhandisi Evarist Ndikilo alisema kuwa kutokana na wajumbe kutoa malalamiko juu ya kampuni hiyo kwenye ujenzi huo ambapo zimepewa kampuni mbili za Skol na Southen Link ni vema wakala wa barabara Nchi Tanroads kuliangalia kwa kina suala hilo.
Ndikilo alisema kuwa kuna haja sasa ya mkataba wake kuangaliwa ikiwezekana kazi hiyo ipewe kampuni nyingine ili iendelee na ujenzi huo kutokana na kampuni hiyo kutoonyesha uwezo.
"Nitafanya ziara kutembelea ujenzi wa barabara hiyo ili kujionea hali halisi ya ujenzi huo ambapo ujenzi huo wa kilometa tano zimepewa kampuni hizo lakini kipande walichopewa kampuni hiyo ya Skol bado hakijajengwa kabisa," alisema Ndikilo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Assumter Mshama alisema kuwa ujenzi huo unakatisha tamaa kutokana kutoonyesha kama kuna kinachofanyika kwenye eneo alilopewa mkandarasi huyo.
Mshama alisema kuwa ucheleweshaji wa ujenzi huo itachelewesha utekelezaji wa muda wa ujenzi wa mradi huo ambao unajengwa kwa awamu.
Naye meneja wa Wakala wa barabara Tanroads mkoa wa Pwani Mhandisi Yudas Msangi alisema kuwa kwa sasa wamewasiliana na makao makuu yao kupitia kitengo cha masuala ya kisheria ili kuangalia mkataba huo ikiwezekana wavunje mkataba huo.
Msangi alisema kuwa tayari wamemuandikia barua nne kuhusiana na uwezo wake lakini inaonyesha kama kuna tatizo hivyo wanaendelea na hatua mbalimbali ili kumalizana naye.
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Kibaha Mjini Silvestry Koka alisema kuwa barabara hiyo ni muhimu sana kwani inaunganisha wilaya za Kibaha na Bagamoyo.
Mbunge wa jimbo la Bagamoyo Dk Shukuru Kawambwa alisema kuwa barabara hiyo ni mbaya sana kwani imeharibika kwa kiasi kikubwa hivyo ni vema wakandarasi hao wakaongeza nguvu ili kukamilisha ujenzi huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.