WAkazi zaidi ya 3,500 wa Mitaa ya Mwanalugali A na B Kata ya Tumbi Wilaya ya Kibaha Mkoani Pwani, wanatarajia kuondokana na kero ya kutembea umbali wa kilometa 10 kufuata huduma za afya kituo cha afya Mkoani na hospital ya Rufaa ya Tumbi baada ya ujenzi wa Zahanati ya Mwanalugali kukamilika mwezi Septemba mwaka huu.
Hayo yamebainika wakati Mkuu wa MKOA wa Pwani Abubakar Kuenge alipotembelea mradi wa miundombinu ulioibuliwa na wananchi na kufadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya jamii (TASAF) katika eneo hilo na kutoa agizo kwa mganga Mkuu wa mkoa kuhakikisha wanaandaa wataalamu na watendaji wa afya mapema ili mradi ukianza wawepo tayari kutoa huduma.
Katika ziara yake hiyo, RC Kunenge alitoa agizo la idara ya Afya kuhakikisha kuwa kunakuwepo vifaa tiba ili huduma zianze Mara moja baada ya ukamilishaji wa mradi huo.
Pia Kunenge alitoa agizo kwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha na wataalamu wake kupima na kuandaa mchoro na Hati kwa eneo hilo ili kuondoa changamoto za migogoro ya ardhi.
Pamoja na hayo, Mkuu huyo wa Mkoa ameitaka Mamlaka ya maji na usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) na Shirika la Umeme (TANESCO) kuweka Mazingira mazuri ya upatikanaji wa huduma hizo huku akiielekeza TARURA kuhakikisha inachonga barabara zote zinazoelekea katika Zahanati ya Mwanalugali ili kuondoa usumbufu.
Awali, mkazi wa Mwanalugali Frida Mvalla alisema mradi huo utakuwa mkombozi kwao kwani walikuwa wakipata shida hasa wajawazito na Watoto pamoja na kuhangaika endapo kunatokea wagonjwa nyakati za usiku.
Nae Mratibu wa TASAF Halmashauri ya Mji wa Kibaha Anita Lioka alisema wananchi wameibua mradi huo na TASAF imefadhili na utagharimu kiasi cha sh. milioni 113.6. hadi kukamilika.
Wakazi wa eneo hilo pia wameomba kuongezwa jengo la kujifungulia ili kusaidia wakinamama na watoto.
Ujenzi huo ulioanza mwezi machi mwaka huu umefikia asilimia 70 ya utekelezaji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.