Zaidi ya sh milioni 900, zimetafunwa na watu wanaodaiwa kuwa ni madalali na baadhi ya viongozi wa vitongoji wakati wa mauziano ya viwanja vya eneo la serikali la Mitamba shamba namba 34 lililopo Kata ya Pangani, Halmashauri ya Mji Kibaha mkoani Pwani.
Mkuu wa mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ametoa kauli hiyo Novemba 3, 2023 kwenye kikao kilichowahusisha waandishi wa habari wa mkoa huo, wakuu wa wilaya, watalaam na wakurugenzi kutoka Halmashauri mbalimbali, kilichokuwa na lengo la kuwasilisha taarifa za utatuzi wa migogoro hasa ya ardhi.
Amesema eneo la Mitamba likiwa na shamba namba 34, lenye ukubwa wa hekta 4000 lilivamiwa na wananchi na kuendeleza shughuli zao.
Amesema maamuzi ya baraza la mawaziri lililokuwa na kazi maalumu ya kushughulikia migogoro ya ardhi nchini liliagiza waliovamia eneo hilo kuondoka mara moja.
Amesema licha ya kuwepo kwa uhalali wa serikali kupitia Wizara ya mifugo kumiliki eneo hilo lakini madalali waliendelea kuwauzia viwanja wananchi.
Hata hivyo, hivi karibuni katika mkutano wake na wananchi wa Kata ya Pangani, Kunenge alitoa muda wa siku 14 kukamatwa viongozi 24 wakiwemo mabalozi, wenyeviti wa mitaa, watendaji walioshirikiana na madalali waliohusika kuwauzia wananchi viwanja katika eneo la shamba namba 34 la Mitamba mali ya Wizara ya mifugo na uvuvi.
Kunenge alisema, anayo orodha ya majina ya viongozi na madalali waliohusika kuwauzia kinyemela wananchi viwanja katika eneo hilo ambalo linamilikiwa na serikali na kwamba anayakabidhi kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU pamoja na Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria.
Aidha Kunenge alitoa agizo kwa Halmashauri ya Mji Kibaha, kupima eneo la shamba Namba 34 la Mitamba lenye ukubwa wa hekta 4000 na kubainisha mipaka yote na matumizi yake ili ijulikane kama vile eneo la ujenzi wa ofisi za umma na huduma za kijamii, makazi kabla ya kuanza oparesheni ya kuwaondoa wananchi walio ndani ya shamba hilo.
“Hekta 2963 kati ya 4000 zimerejeshwa kwa Halmashauri ya Mji Kibaha kwa ajili ya kutumika kwenye shughuli za maendeleo na kubakiwa na eneo la hekta 1037 ambazo hadi sasa zimebaki kwa Wizara ya Mifugo kwa ajili ya kufanya shughuli zake,” amesema Kunenge.
Siku chache zilizopita, alipozungumzia historia ya eneo hilo, Mpimaji Ardhi Halmashauri ya Mji Kibaha, Aron Shushu, alisema kiwanja hicho kilipimwa upya kwa kuzingatia sheria namba 8 ya mipango miji na kwamba mwaka 2021 kilifanyika kikao na wananchi hao kwa ajili ya kutoa katazo la kutovamia shamba hilo.
Katika taarifa yake Kunenge, amesema tayari waliohusika na utapeli wa kuuza shamba namba 34 wameanza kuripoti kwenye vyombo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya hatua za kisheria.
Aidha amesema baadhi ya wananchi ni waoga kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kuwashughulikia wale wote madalali waliouza kinyemele ardhi inayomilikiwa na serikali.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.