Wananchi wa Mkoa wa Pwani wametahadharishwa kujikinga na ugonjwa wa homa ya Dengue ambapo hadi sasa kuna wagonjwa 42 wanaougua ugonjwa huo.
Hayo yalisemwa mjini Kibaha na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo kwenye kikao maalumu cha kamati ya ulinzi na usalama na wadau mbalimbali wakiwemo kamati ya amani inayoundwa na viongozi wa madhehebu mbalimbali na viongozi wa afya na Wilaya ambazo zimeguswa na ugonjwa huo.
Ndikilo alisema kuwa uwepo wa ugonjwa huo uliripotiwa Mei 8 mwaka huu ambapo mgonjwa wa kwanza alibainika wilayani Kibaha ambaye alitokea Ubungo Msewe Jijini Dar es Salaam.
"Wilaya inayoongoza kuwa na wagonjwa wengi wa ugonjwa huu ni Mkuranga ambapo ina wagonjwa 35, Rufiji 4 na Kibaha 3 hali ambayo wananchi na wataalamu wa afya washirikiane ili kuuwa mbu na mazalia yao," alisema Ndikilo.
Alisema kuwa ili kukabiliana na ugonjwa huo viongozi wa dini wanapaswa kutoa elimu juu ya ugonjwa huu pia vipeperushi vya ugonjwa huo viwekwe kwenye mbao za matangazo,maofisi mbalimbali na sehemu zenye watu wengi.
Kwa upande wake mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Dk Gunini Kamba alisema kuwa ugonjwa huo unasambaa kwa kasi hivyo wananchi wanapaswa wachukue tahadhari.
Dk Kamba alisema kuwa vipimo kwenye vituo vya afya serikali gharama zake ni bure na kwa vile vya watu binafsi zisizidi 15,000.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Assumter Mshama kuwa elimu itolewe sehemu mbalimbali hasa zile zenye mikusanyiko ya watu ili wapate uelewa juu ya ugonjwa.
Pia Mkuu wa Wilaya ya Kibaha mstaafu Halima Kihemba alisema kuwa kuwe na utaratibu wa uchafu unaokusanywa sehemu mbalimbali kutupwa sehemu husika ili kupunguza mazalia ya mbu.
Homa ya dengue hutokana na mtu kuumwa na mbu aina ya Aedes mwenye virusi vya ugonjwa huo ambao unaweza kuhatarisha maisha ya watu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.