Mkoa wa Pwani umepokea ujumbe wa washiriki kutoka Chuo cha Ulinzi cha Taifa (NDC) ambao wamewasili mkoani hapo kwa lengo la kufanya ziara ya mafunzo ya kiusalama inayohusisha masuala ya kiuchumi, kijamii, kisiasa, na uwekezaji.
Ziara hiyo, iliyoanza Januari 13, 2025, imejumuisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi na kuongozwa na Brigedia Jenerali Charles James Ndiege, Mkufunzi Elekezi Mwandamizi wa Jeshi la Nchi Kavu kutoka NDC, pamoja na wakufunzi wengine.
Lengo kuu la ziara hiyo ni kuwajengea washiriki uelewa wa changamoto na fursa zilizopo mkoani Pwani.
Akizungumza wakati wa kuwapokea wageni hao, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mheshimiwa Abubakar Kunenge, alisema kuwa ziara hiyo ni fursa ya kipekee kwa washiriki kujifunza mambo mbalimbali katika nyanja za kisiasa, uchumi, kijamii, na uwekezaji.
“Ujio wa washiriki hawa sio tu unaimarisha ushirikiano wa kimataifa, bali pia unachangia kukuza maendeleo ya Mkoa wa Pwani na kuimarisha hali ya ulinzi na usalama,” alisema Kunenge.
Aidha, alibainisha kuwa Mkoa wa Pwani unaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia vipaumbele vya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa katika masuala ya maendeleo ya viwanda na uwekezaji.
Kwa upande wake, Brigedia Jenerali Charles James Ndiege alisema lengo la ziara hiyo ni kujifunza masuala ya kiusalama katika nyanja za kiuchumi, kijamii, kisiasa, na viwanda, ambavyo vina athari kubwa kwa usalama wa nchi. Alieleza kuwa Mkoa wa Pwani umechaguliwa kwa kuwa unaongoza kwa kuwa na viwanda vingi na mazingira mazuri ya uwekezaji, jambo ambalo linachangia kukuza uchumi wa taifa.
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Kanal Richard Rama alisema kuwa wamejifunza jinsi Mkoa wa Pwani ulivyoweka kipaumbele katika uchumi kupitia uwekezaji katika viwanda na miradi mingine ya maendeleo.
Washiriki hao wanatarajiwa kukaa mkoani Pwani kwa siku tano, ambapo watatembelea maeneo mbalimbali na kushuhudia shughuli za uzalishaji mali.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.