Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo amewataka wafanyabiashara wote Mkoani Pwani kuacha mara moja tabia ya kuficha bidhaa ili zionekane adimu na waweze kupandisha bei kwa manufaa yao binafsi.
Kauli hiyo ameitoa jana pindi alipofanya ziara ya kushtukiza katika maghala ya kuhifadhia bidhaa mbalimbali za wafanyabiashara waliopo Mailimoja Mjini Kibaha kwa lengo la kuangalia bidhaa za sukari na mafuta ya kula kama zipo ambapo alibaini bidhaa hizo zipo za kutosha .
“Natoa tahadhari kama kutakuwa na mfanyabiashara yeyote ambae pengine atajaribu kuficha hizi bidhaa zionekane adimu na zipande bei kwa lengo la kijitafutia utajiri wa haraka haraka ajue kwamba atakumbana na mkono wa sheria na ajue kwamba Serikali ya Mkoa itamchukulia hatua kali sana”alisema Ndikilo.
Aidha Mhandisi Ndikilo amewatoa wasiwasi wananchi wa Mkoa Pwani, kwa kuwahaikikishia kuwa bidhaa ya sukari na Mafuta zipo za kutosha na suala la kuadimika na kupanda bei kwa bidhaa hizo halitakuwepo.
Naye mwenyekiti wa jumuia ya wafanyabiashara Mkoa Pwani Abdalla Ndauka amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa mkoa kuwa wao wapo bega kwa kwa bega na Serikali ya Mkoa katika kuhakikisha kuwa bidhaa hizi zitapatikana kwa wingi na pia hawataruhusu suala kuficha bidhaa hizi.
“Nawahakikishia wananchi wa Mkoa Pwani kuwa kwa ushirikiano ambao tumekuwa nao kati yetu na Serikali, nitahakikisha wananchi watapata huduma kama kawaida na nitahakikisha kwamba suala hili halitaokea na endapo atatokea mwenzetu ndani ya chama ambae ataenda kinyume na haya basi tutamshughulikia sisi wenyewe kwanza kama chama.
Na nawaomba wafanyabiashara wote wa Mkoa Pwani tuhakikishe kuwa huduma zote za msingi ambazo tulikusudia kuzitoa kwa wananchi basi tuzitoe kwa wakati bila kujali huyu ni nani hasa katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani”alisema Ndauka .
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.