Mafunzo ya matumizi ya Mfumo wa Integrated Monitoring and Evaluation System (iMES) yamefanyika mkoani Pwani kwa lengo la kuwawezesha Maafisa Watendaji wa Vijiji na Mitaa kukusanya taarifa mbalimbali zenye mlengo wa kijinsia. Mafunzo haya yamefanyika kupitia Mradi wa Women’s Leadership and Economic Rights Project (WLER) unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Rais – TAMISEMI na Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake (UN Women).
Mafunzo hayo ya siku tano yamefanyika kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 3, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kibaha. Washiriki walitoka katika Halmashauri za Chalinze, Kisarawe na Manispaa ya Kibaha.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Pwani, Bi. Grace Tete, alisema lengo kuu ni kuwajengea uwezo Maafisa Watendaji wa Vijiji/Mitaa 32 katika ukusanyaji na uingizaji wa taarifa sahihi kwenye mfumo wa iMES ili kusaidia kupanga na kufuatilia utekelezaji wa shughuli za maendeleo zenye kuzingatia usawa wa kijinsia.
“Kupitia mfumo huu, taarifa zitapatikana kwa urahisi na kwa wakati, jambo litakalosaidia kupanga maendeleo yanayolenga wanawake, wasichana na watu wenye ulemavu kwa ufanisi zaidi,” alisema Tete.
Washiriki wa mafunzo hayo walijumuisha Maafisa TEHAMA mmoja kutoka kila Halmashauri, Maafisa Maendeleo ya Jamii watatu kutoka kila Halmashauri, Maafisa Maendeleo ya Kata kutoka maeneo ya utekelezaji wa mradi (Msoga, Ubena, Pangani, Mkuza, Kisarawe na Masaki), pamoja na Maafisa Watendaji wa Vijiji/Mitaa 32.
Mradi wa WLER, unaofadhiliwa na UN Women, ulianza kutekelezwa mwaka 2022/2023 katika kata tisa za Mkoa wa Pwani, kwa lengo la kuhakikisha wanawake na watu wenye ulemavu wanashiriki kikamilifu katika vyombo vya maamuzi na kupata fursa mbalimbali za kiuchumi.
Mafunzo hayo yalijumuisha vipindi vya nadharia darasani na mafunzo kwa vitendo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi na kuboresha hali zao za kiuchumi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.