“Uendeshaji wa michezo kama hii na mashindano kama haya kunahitaji uwekezaji mkubwa na changamoto za kibajeti ni nyingi , hata hivyo uwekezaji huu ni muhimu sana katika maendeleo ya Mkoa wetu hivyo hatuna budi kuwekeza katika michezo ili kuwajengea vijana wetu misingi bora katika suala zima la michezo na hatuna budi kufanya hivyo ,na tunakila sababu kufanya hivyo.”
Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Mkoa Pwani ndugu Zuberi Samataba wakati akifungua mashindano ya UMISETA Mkoa Pwani katika viwanja vya shulerya Filbert Bayi vilivyopo mjini Kibaha.
Akifungua mashindano hayo Samataba aliwataka wanamichezo hao ambao ni wanafunzi wa shule za sekondari za Mkoa Pwani kuwa na nidhamu kwa kipindi chote cha mashindano hayo.
Katika kuendeleza suala zima la michezo Mkoa wa Pwani Katibu Tawala Samataba amezitaka Halmashauri zote za Mkoa Pwani kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya uendeshaji wa michezo ili kuweza kusaidia kuwa na timu bora ambayo itaweza kuleta matokeo mazuri katika michezo.
Samataba alisema kuwa “tukiwa na bajeti ya kutosha ya kuendesha michezo nina amini maandalizi na mashindano yatakuwa mazuri katika ngazi ya Halmashauri na Mkoa.”
Aidha amewataka maafisa Michezo na Utamaduni na Walimu wa michezo kutumia vyema taaluma zao katika kuendeleza michezo Mkoani Pwani. Hata hivyo aliwataka wakurugenzi wawawezeshe maafisa hao na walimu wa michezo katika kuendeleza taaluma zao ili waweze kuleta sifa kimkoa na Kitaifa kwa ujumla.
Katika hatua nyingine Samataba alisema kuwa mkoa wa Pwani sasa upo katika utekelezaji wa sera ya viwanda hivyo amewataka wanamichezo hao kuongeza juhudi katika michezo na taaluma nyingine ili kuweza kujipatia ajira mbalimbali katika viwanda hivyo.
Michezo ya umiseta Mkoa wa Pwani imeshirikisha Halmashauri zote za Mkoa Pwani na imeanza rasmi tarehe 26 Mei 2018 na inatarajia kumalizika tarehe 28 Mei 2018 na imejumuisha michezo mbalimbali ikiwemo Mpira wa Miguu kwa wavulana na wasichana,Mpira wa mikono kwa Wavulana na wasichana,Mpira wa wavu wavulana na wasichana ,Mpira wa kikapu wavulana na wasichana ,mpira wa pete wasichana tu,Riadha wavulana na Wasichana , Sanaa za maigizo , Ngoma na Mashairi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.