WaziriI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Angela Kairuki,amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge pamoja na Wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanafuatilia ufundishaji wa walimu ili kuweza kuboresha elimu
Pamoja na hilo lakini pia amewataka viongozi hao kushughulikia changamoto na kero za walimu hususani katika kuwalipa stahiki zao ikiwemo fedha za malimbizo ya mishahara na madeni mbalimba ili waweze kufanya kazi zao kwa umahiri.
Kairuki,ametoa maagizo hayo katika kikao kazi cha mapitio ya tathimini ya utekelezaji wa shughuli za uboreshaji na usimamizi wa elimu kwa mwaka 2022 na mpango wa mwaka 2023 kilichofanyika katika viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha.
Katika kikao hicho kilichowakutanisha maafisa mbalimbali wa elimu kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Pwani,Wakurugenzi wa Halmashauri ,maafisa elimu Kata,Wakuu wa Shule pamoja na viongozi wengine kilikuwa na lengo la kukumbushana namna ya kuboresha elimu ya Msingi na Sekondari.
Kairuki, alisema kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imefanyakazi kubwa katika kuboresha mazingira ya ufundishaji kwa walimu na hata kutatua changamoto nyingine.
Aidha ,Kairuki amemshukuru Rais Samia kwa jitihada hizo maana angeweza kuingia madarakani na kufuta mpango wa elimu bure lakini cha ajabu katika kipindi kifupi cha Novemba 2021 na Desimba 2022 ameendeleza zaidi mpango huo na kuweza kujenga madarasa 23000 .
Kairuki, ameongeza kuwa pamoja nakujenga madarasa hayo lakini bado ameendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kujenga Shule mpya katika Mikoa mbalimbali hapa nchini zikiwemo Shule za Sekondari za wasichana
"Tumeona jinsi ambavyo Rais wetu anavyofanyakazi hususani katika sekta hii ya elimu kwahiyo niwaombe tuendelee kuyasemea mafanikio haya ili kuweza kumtia moyo Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa
Kairuki ,pamoja na mafanikio makubwa yaliyopo lakini bado zipo changamoto mbalimbali ikiwemo watoto wa awali kushindwa kusoma na kuandika ,pamoja na wanafunzi wanaoingia kidato cha kwanza kushindwa kuongea lugha ya kiingereza.
Alisema,sio changamoto hiyo tu lakini kuna sababu za kimila na desturi pamoja na utoro zinazosababisha watoto kushindwa kufikia malengo na kwamba amewataka maafisa hao kubuni mikakati sahihi ya kuthibiti changamoto hizo.
Mbali na kikao hicho lakini pia Kairuki akiwa Mkoani Pwani alitembelea na kukagua Shule ya Sekondari Sofu pamoja iliyopo Mjini Kibaha na kufuruhishwa na ujenzi huo huku akiwataka walimu kusimamia vyema miundombinu ya Shule hizo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge,alisema kuwa tayari Mkoa ulishafanya kikao kama hicho na utekelezaji wake umekwenda vizuri.
Kunenge,alisema kuwa walifanya tathmini na kubaini Mkoa wa Pwani Kuna Mila na desturi na tathmini hiyo ilikuwa pamoja na kuwauliza wanafunzi kama Kuna utaratibu wa masomo wanapofika nyumbani,vitabu na vifaa vingine vya kujisomea.
Aidha, Kunenge amempongeza Rais wa awamu ya Sita Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya hasa katika kutambua masuala mbalimbali ya elimu yaliyopo Mkoani Pwani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.