Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete (Mb), Januari 24, 2026, amezindua jengo jipya la Ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika Wilaya ya Chalinze, Mkoa wa Pwani.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Kikwete amewataka watendaji wa taasisi za umma nchini kutoa kipaumbele kwa wakandarasi wa maeneo husika katika utekelezaji wa miradi ya Serikali, akisema hatua hiyo itachangia kukuza uchumi wa wananchi na kuharakisha maendeleo katika maeneo yanapotekelezwa miradi hiyo.
Ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha utawala bora na matumizi sahihi ya rasilimali za umma, huku akipongeza TAKUKURU kwa usimamizi makini wa fedha za umma uliowezesha kurejeshwa kwa zaidi ya shilingi bilioni 60.2 kupitia operesheni mbalimbali zilizotekelezwa nchini.
Vilevile, Waziri Kikwete amewahimiza watumishi wa TAKUKURU na watumishi wengine wa umma kutunza majengo ya ofisi na vifaa vilivyopo, pamoja na kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na weledi ili kufanikisha azma ya Serikali ya kujenga Tanzania isiyo na rushwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Crispin Chalamila, amesema ujenzi wa jengo hilo umegharimu jumla ya shilingi milioni 406.49 hadi kukamilika kwake.
Amefafanua kuwa TAKUKURU ilitenga zaidi ya shilingi milioni 414 kwa ajili ya ujenzi huo, lakini kutokana na kuzingatia misingi ya maadili, uwajibikaji na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, taasisi hiyo ilifanikiwa kutumia kiasi cha shilingi milioni 406.49 pekee, hali iliyopelekea kubaki kwa zaidi ya shilingi milioni nane ambazo zitatumika katika utekelezaji wa shughuli nyingine za maendeleo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.