Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wananchi waliokumbwa na adha ya mafuriko nchini waendelee kuwa watulivu wakati Serikali ikiendelea kuratibu utoaji wa misaada kwenye maeneo yaliyoathirika.
“Barabara ya Mkongo hadi Utete na ile ya kutoka Mloka Mkongo zote zimeathirika. Tunafanya kazi ya kurejesha mawasiliano ili wananchi waweze kupata huduma muhimu,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa wito huo Aprili 16, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Chumbi, wilayani Rufiji, mkoani Pwani ambako alikwenda kukagua athari za mafuriko kwenye eneo hilo. Hadi sasa waathirika 740 wako kambini.
Waziri Mkuu ambaye aliwasili Ikwiriri, Rufiji akitokea Mlimba, Morogoro aliwaomba wananchi hao waendelee kutulia kwani serikali iko nao na itaendelea kuwahudumia hadi hali yao irejee katika hali ya kawaida.
“Naomba mpokee salamu za pole kutoka kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, tunatambua kuna watu wamepoteza mali na wengine mifugo,” amesema.
Amewataka watendaji wa vijiji waendelee kubaini maeneo mapya ya kuishi ambayo yatatumika kuhamisha kaya zilizoathirika. “Watendaji wa vijiji tuainishe maeneo mapya ya kwenye miinuko ili baadaye watu waweze kuhamishiwa huko,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameziagiza TARURA, TANROADS na TAZARA zishirikiane kufanya ukarabati katika maeneo yote yaliyopata athari wakati Serikali inasubiri kumalizika kwa mvua ili iweze kufanya ukarabati mkubwa.
Waziri Mkuu amefuatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dkt. Selemani Jaffo, Naibu Waziri wa Nchi (OWM-SBU) Bi. Ummy Nderiananga, Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Mobhare Matinyi na watendaji wengine.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar kwa upande wake amesema kwamba ghgfhMkoa unaendelea kutoa huduma mbalimbali za kijamii kwa waathirika wa mafuriko hayyo na tayari kituo cha Afya cha Muda kimeanzisha katika kata ya Mohoro ambapo wananchi wanapata hapo huduma za Afya.
Ameeleza kuwa tayari Mkoa umeshaanza kufanya tahmini ya kina ya athari ya mafuriko hayo.
Katika hatua nyingine Kunenge ameishukuru serikali na wadau mbalimbali kwa kuweza kutoa misaada ya kibinadamu kwa waathirika wa mafuriko Wilayani Kibiti na Rufiji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.