Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Kassim amezitaka Serikali za Vijiji na ngazi nyingine Mkoani Pwani kujikita katika kuimarisha ulinzi kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo ya viwanda ili kulinda mali na usalama wa wawekezaji na watanzania kwa ujumla.
Amesema haijajulikana hadi sasa nia na dhamira ya watu wasiojulikana wanaojihusisha kupoteza maisha ya watu na ni hatari endapo watajiingiza katika maeneo ya uwekezaji kwani hakuna mwenye uhakika wa azma yao. Alieleza kuwa ni jukumu la kila mmoja kusimamia kulinda nchi kuanzia maeneo wanayoishi
Aidha Waziri Mkuu, ametoa wiki mbili kwa Waziri wa Maji kutathmini matokeo ya mwenendo wa mradi wa maji wa WAMI, ili kutoa utaratibu na kama sheria inaruhusu kuvunja mkataba ikiwa Mkandarasi ameshafikia kiwango cha asimilia 50 ya utekelezaji.
Pia ameziagiza Halmashauri nchini kuona umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili ya kununua magari ya zimamoto yatakayosaidia kudhibiti majanga ya moto yanapotokea hususani kwenye maeneo ya uzalishaji na viwanda.
Katika hatua nyingine ameyataka mashirika ya TANESCO na DAWASCO kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya umeme na maji katika maeneo yenye uwekezaji ili kuvutia wawekezaji.
Alitoa rai hiyo, wakati wa ziara yake ya siku moja ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza sabuni cha KEDS kilichopo Kibaha,na kiwanda cha kutengeneza vigae TWYFORD Ceramics Co. Ltd kilichopo kata ya Pingo - Chalinze
Aliendelea kusema kuwa Serikali imejipanga kuendelea kusimamia amani na utulivu, ambapo amewataka wananchi waiunge mkono Serikali kupambana na wahalifu wasio na nia njema na Serikali.“Hatuna uhakika kwa watu hawa wanaofanya vitendo vya ovyo, watanzania waungane na Serikali katika kupambana ili wasije kuingia kwa wawekezaji na kupoteza ndoto za Serikali za kupata wawekezaji “alisema Majaliwa.
Akizungumzia tatizo la uhaba wa maji, alisema mradi wa WAMI ulikuwa ukamilike tangu mwezi July mwaka huu.
Alisema alitembelea mradi huo mwezi juni mwaka huu ukiwa chini ya asilimia 38 na kusema mkandarasi akiendelea kusuasua watamfukuza na kutoa agizo ikifika mwezi huu wafikie asimilia 80.
“Nilitaka kuja mwezi huu lakini nikaambiwa spidi ni ndogo na bado hali hairidhishi, na mkandarasi hajamaliza”mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete amekuwa akiuliza juu ya kukwama kwa mradi huo” ;”Nimetoa wiki mbili kwa waziri aangalie dhamana ya kampuni kwenye ubalozi wao wa India na kuangalia sheria namna ya kufanya ama kukamilisha mradi kwa muda mfupi uliobaki”alifafanua.
Kuhusu nishati ya umeme Majaliwa, alisema Serikali ipo mbioni kutekeleza mradi mkubwa wa umeme Stiegler’s Gorge katika chanzo cha mto Rufiji, utakaozalisha Megawatts 2,100 zitakazoondoa kama si kumaliza upungufu wa umeme uliopo.
Aliitaka Halmashauri ya Chalinze, ijipange kwa matumizi bora ya ardhi ili kuondoa migogoro na kuondoa usumbufu kwa wawekezaji.
Kuhusu suala la zimamoto, Mhe. Majaliwa alisema Mkoa huu kwasasa una viwanda vikubwa hivyo wakati Serikali ikipokea changamoto ya uhaba wa vifaa na magari ya zimamoto, Halmashauri ijipange kupitia bajeti zao.
“Viwanda hivi ni vikubwa vinajengwa, kiwanda hiki cha KEDS kina jengo hilo hapo lenye urefu wa mita 30 juu, tuombe mungu moto usitokee, unawezaje kuzima moto kwa maji ya kwenye ndoo, ipo haja ya kuangalia namna ya kutatua changamoto hii”
Kwa upande wa miundombinu ya barabara, alitoa rai kwa Halmashauri ya Mji wa Kibaha kuboresha barabara zilizopita mitaani na kuhakikisha mitaa yote iwe na barabara bora kwa kufumua zisizofaa na kuchonga barabara zenye viwango.
Pamoja na hayo, Majaliwa alibainisha uwekezaji kama huu unaendana na dhana ya Rais Mhe Dkt. John Pombe Magufuli wa kuifanya nchi kuwa ya viwanda ambapo itaongeza pato la nchi na itazalisha ajira kwa wingi.
Aliwasihi vijana ambao tayari wana ajira kwenye viwanda hivyo kutumia nafasi walizozipata kwa kuchapa kazi .
Majaliwa aliwaomba vijana hao kuchapa kazi na kuwathibitishia wawekezaji kuwa watanzania ni wachapazi na wana uwezo wa kufanya kazi viwandani na hakuna haja ya kuleta watumishi nje ya nchi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo, alimwambia Waziri Mkuu, kwamba Mkoa huu unakabiliwa na changamoto ya miundombinu ya barabara isiyo ya kuridhisha kwa wawekezaji.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa nishati ya umeme isiyokidhi mahitaji kwani kwasasa mahitaji ni Megawatts 73.2 na uliopo ni Megawatts 40 hautoshelezi mahitaji.
Mhandisi Ndikilo, alieleza tatizo la uhaba wa vifaa, vitendea kazi na magari kwa idara ya zimamoto na kuhofia endapo janga la moto litatokea inaweza ikatokea kushindwa kuzima moto kwa wakati na kusababisha athari kubwa.
Wakati huo huo, Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha KEDS na TWYFORD Bw. Jack Feng alisema asilimia 95 ya malighafi itakuwa inatoka hapa nchini. Alisema, katika kiwanda cha KEDS wameshaajiri watu 200 huku wakitarajia kuajiri wafanyakazi 2,000 katika kiwanda hicho.
"Ndani ya ujenzi huu kuna kiwanda kingine kikubwa ambacho tutazalisha pempars na kiwanda kingine tutatengeneza misumari” alieleza Bw. Feng.
Alisema hatua ya ujenzi ni nzuri imefikia asilimia 90 na wanategemea kuanza uzalishaji mwezi ujao. Mradi wa ujenzi wa kiwanda hicho utagharimu dola mil.200 hadi utakapokamilika.
Bw. Feng alifafanua kuwa kwenye kiwanda cha TWYFORD watarajia kuajiri wafanyakazi 4,000 hadi 6,000 mara watakapoanza kuzalisha mwezi novemba mwaka huu, 2017.Sasa kuna wafanyakazi 1200. Watauza vigae ndani ya nchi hadi nje ya nchi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.