Zaidi ya ajira 4,000 zinatarajiwa kuzalishwa katika Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo kufuatia kukamilika kwa taratibu za ndani za upatikanaji wa ardhi na maandalizi ya mikataba kati ya Mamlaka ya Eneo Maalum la Uwekezaji Tanzania (TISEZA) na makampuni sita (6) yatakayotekeleza miradi ya kimkakati ndani ya Eneo Maalum la Uchumi la Bagamoyo Eco Maritime City (BEMC SEZ).
Miradi hiyo inalenga kuimarisha uzalishaji wa viwandani, kuongeza mauzo ya nje, kuhamisha teknolojia na ujuzi pamoja na kukuza ajira hususan kwa vijana, sambamba na kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii Bagamoyo na maeneo jirani.
Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA), Gilead Teri, katika hafla fupi ya makabidhiano ya hati za mikataba ya uwekezaji kwa wawekezaji waliopatiwa maeneo katika Eneo Maalum la Uchumi la Bagamoyo Eco Maritime City (BEMC SEZ), sambamba na utoaji wa taarifa ya hali ya uwekezaji nchini kwa mwaka 2025.
Alisema Miongoni mwa makampuni hayo ni Canary Industries Limited, inayopanga kuwekeza takribani shilingi bilioni 1 kwa kuanzisha kiwanda cha kisasa cha vifungashio vya chakula (PET na PP) katika eneo la ekari moja Bagamoyo. Mradi huo unalenga kuongeza thamani ya uzalishaji wa ndani, kupunguza uagizaji wa bidhaa kutoka nje na kukuza mauzo ya nje hususan katika masoko ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Alifafanua kuwa Grosso Engineering and Fabricators Limited, inapanga kuwekeza dola za Marekani milioni 5.2 kuanzisha karakana ya utengenezaji wa vyuma, kuunganisha mashine za kilimo pamoja na kiwanda cha hot-dip galvanizing. Mradi huu unatarajiwa kuzalisha ajira zaidi ya 100 za kudumu na ajira 200 za muda, na kuimarisha sekta ya uhandisi nchini.
Alisema kuwa Kwa upande wa kampuni ya Jaribu Cashews Production Limited, itawekeza dola za Marekani milioni 5 katika uchakataji wa korosho, kahawa na viungo kwa ajili ya masoko ya kimataifa, hatua itakayozalisha ajira zaidi ya 140 za kudumu na za muda.
Aliongeza kuwa Novara Global Steel Limited inapanga kuwekeza hadi dola za Marekani milioni 8 katika uzalishaji wa bidhaa za chuma, ambapo takribani asilimia 80 ya uzalishaji inalenga mauzo ya nje, huku mradi huo ukitarajiwa kutoa ajira zaidi ya 100 kwa Watanzania.
Alileza kuwa Katika kuendeleza sekta ya madini na viwanda vizito, Shah Steel Global inapanga kuanzisha kiwanda cha kisasa cha uzalishaji wa Ferro Alloys kwa uwekezaji wa awali wa dola za Marekani milioni 5, mradi unaotarajiwa kutoa ajira zaidi ya 200 na kuingiza mapato ya dola za Marekani milioni 32 hadi 43 kwa mwaka kupitia mauzo ya nje.
Aidha alisema Mradi mkubwa zaidi ni wa MCGA Auto Limited, unaohusisha uwekezaji wa takribani dola za Marekani milioni 50 katika kuunganisha magari kwa ajili ya soko la ndani na la kikanda. Mradi huu unatarajiwa kuzalisha ajira za moja kwa moja kati ya 500 hadi 1,000 na zaidi ya ajira 3,500 zisizo za moja kwa moja.
Kwa ujumla, utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kuleta manufaa makubwa ikiwemo kuongezeka kwa ajira kwa Watanzania, uhamishaji wa teknolojia na ujuzi, kukuza minyororo ya thamani ya ndani, kuongeza mapato ya Serikali na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha uzalishaji na biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.