Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, ambaye pia ni Skauti Mkuu wa Tanzania, Rashid Mchatta, ameongoza kikao kilichofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, kufuatia hitimisho la ziara ya siku tano ya wanafunzi kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC). Ziara hiyo, iliyoanza tarehe 13 Januari 2024 na kuhitimishwa tarehe 17 Januari 2024, imeleta matokeo chanya katika maendeleo ya Mkoa wa Pwani, hasa kwenye sekta za kilimo, usalama, uwekezaji wa viwanda, utalii, elimu, na uongozi.
Akizungumza katika kikao hicho, Rashid Mchatta alieleza kuwa ziara hiyo imeonyesha njia za kuboresha miundombinu ya uzalishaji, kukuza kilimo cha umwagiliaji, kuboresha mazao ya mifugo, na kuongeza matumizi ya teknolojia katika kilimo. Aidha, aliipongeza NDC kwa mchango wao wa kubainisha fursa za kiuchumi na kutoa mapendekezo ya hatua za kuimarisha uchumi wa Mkoa wa Pwani.
“Ziara hii imeleta mwanga mpya wa jinsi ya kuboresha maendeleo ya mkoa wetu, hasa kwa kubaini maeneo muhimu kama utalii, uchumi wa bahari, na uzalishaji wa kilimo kwa tija zaidi,” alisema Mchatta.
Kwa upande wake, Kiongozi wa msafara huo, Brigedia Jenerali Charles James Ndiege, ambaye pia ni Mkufunzi Elekezi kutoka NDC, alisema kuwa ziara hiyo ilikuwa ni sehemu ya mafunzo ya kimatendo baada ya kujifunza nadharia darasani.
“Hii ni ziara ya kimafunzo ili kutekeleza sera za kiusalama, kiuchumi, na kijamii kwa vitendo. Tumechagua Mkoa wa Pwani kwa sababu unaongoza kwa maendeleo ya viwanda nchini. Tumetembelea viwanda mbalimbali na kutoa mapendekezo yetu ya kuboresha zaidi uzalishaji,” alisema Brigedia Jenerali Ndiege.
Aliongeza kuwa walitembelea ofisi za wilaya za Bagamoyo na Chalinze ambapo walijifunza kuhusu masuala ya kijamii, elimu, afya, na huduma za maji, huku wakishuhudia mifano bora ya usimamizi wa fedha unaochochea maendeleo kwa jamii.
Mhandisi Shabani Seleman Kambabhe, mmoja wa washirikiwa mafunzo kutoka NDC, alieleza kuwa ziara hiyo imeongeza maarifa ya washiriki kuhusu jinsi ya kuboresha sera na kuzitekeleza kwa ufanisi.
Ziara hiyo iliwapa washiriki hao nafasi ya kutembelea maeneo ya uzalishaji kama Kiwanda cha kuchata nyama chaTanChoice, Shamba la uzalishaji wa mbegu za Malisho (Vikuge), Kiwanda kuunganisha Magari(GFA), Kiwanda cha kuzalisha Viwatilifu (Tanzania Biotech), Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), Taasisi ya Uzalishaji wa Chanjo za Mifugo (TVI), pamoja na vivutio vya kihistoria kama Kaole na Mji Mkongwe Bagamoyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.