Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa, ametangaza rasmi kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo imepandishwa hadhi na kuwa Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo.
Tamko hilo limetolewa mbele ya maelfu ya wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Nia Njema, ambapo Waziri Mchengerwa alieleza kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo kutoka kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suhuhu Hassan
“Kwa niaba ya Rais wetu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, natangaza rasmi kuwa kuanzia leo, Bagamoyo ni Halmashauri ya Mji. Hii ni fursa kubwa ya maendeleo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyeidhinisha Bagamoyo kuwa mji rasmi kutokana na kasi ya ukuaji wa uchumi na ongezeko la watu.kwa wananchi wa Bagamoyo,” alisema Mchengerwa.
Amesema kuwa tayari ameagiza wataalamu wa mipango kutoka TAMISEMI kufika wilayani humo kwa ajili ya kuanza kazi ya kuandaa mpango wa mji huo kwa kuzingatia sheria na taratibu zote. Vilevile, ameielekeza Ofisi ya Katibu Mkuu TAMISEMI kuandaa tangazo rasmi katika Gazeti la Serikali kwa ajili ya kutangaza kupandishwa hadhi kwa Halmashauri hiyo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mchengerwa ameagiza kutolewa kwa fedha kwa ajili ya kuboresha huduma za afya wilayani Bagamoyo. Ameielekeza Ofisi ya Katibu Mkuu TAMISEMI kuhakikisha kuwa Shilingi milioni 700 zinapelekwa kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya katika eneo la Kisutu na Shilingi milioni 300 zitatolewa kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati mpya katika eneo la Kitame.
Aidha, Waziri Mchengerwa ameielekeza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kufanya mapitio ya mtandao wa barabara katika mji wa Bagamoyo kwa lengo la kuandaa mpango wa kuongeza mtandao wa barabara za lami, ili kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii katika mji huo unaokua kwa kasi.
Akimkaribisha Waziri Mchengerwa, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, alimshukuru Rais Samia kwa mchango wake mkubwa katika kuifungua Bagamoyo na kuiletea maendeleo makubwa katika kipindi kifupi.
“Sisi wakazi wa Bagamoyo tunamshukuru sana Mhe. Rais Samia. Ameridhia ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, ameridhia reli ya SGR kutoka Bagamoyo hadi Kwala kwa ajili ya mizigo, pia tumeona ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha megawati 22 kilichopo Chalinze, na sasa ujenzi wa barabara ya Makofia–Mlandizi kwa njia mbili umeanza,” alisema Mhe. Kunenge.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.