Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, ameanza rasmi ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, ikiwa ni sehemu ya mwendelezo wa kutembelea halmashauri zote za Mkoa wa Pwani kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kufanya vikao kazi na watumishi wa umma.
Akiwa Kisarawe, Katibu Tawala ametembelea miradi minne ya maendeleo na kueleza kuridhishwa kwake na namna miradi hiyo ilivyotekelezwa. Aidha, amempongeza na kumshukuru Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mhe. Petro Magoti, kwa ushirikiano mkubwa aliouonesha katika kufanikisha ziara hiyo.
Katika kikao na watumishi wa halmashauri, Mnyema amewataka kufanya kazi kwa weledi, kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Ameeleza kuwa watumishi wana wajibu wa kuwatumikia wananchi kwa uaminifu na kusaidia kufanikisha malengo ya Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akizungumzia ukusanyaji wa mapato, Katibu Tawala aliipongeza halmashauri kwa kuvuka malengo ya makusanyo ndani ya miaka miwili iliyopita, lakini akasisitiza haja ya kubuni mbinu mpya za kuongeza mapato zaidi.
"Kisarawe ina uwezo mkubwa wa kukusanya mapato kuliko inavyokusanya sasa. Tukiunganisha nguvu, tunaweza kuinua halmashauri yetu kwa kiwango kikubwa zaidi,” alisema Mnyema.
Amesisitiza pia kuwa fedha zinazotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo zisimamiwe kwa uadilifu na miradi hiyo ikamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyokubalika.
Ziara ya Katibu Tawala wa Mkoa itaendelea katika Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.