Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, ameanza ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mafia leo, Agosti 14, 2025, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kutembelea Halmashauri zote za Mkoa wa Pwani. Lengo la ziara hiyo ni kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kufanya vikao kazi na watumishi wa Halmashauri husika.
Akiwa katika ziara hiyo, Mnyema amewataka viongozi wa Halmashauri ya Mafia kujifunza kutoka maeneo mengine yenye mazingira yanayofanana kijografia lakini yamepiga hatua kubwa kiuchumi, ili kuboresha ubunifu wa miradi na kuongeza mapato ya Halmashauri.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kukamilisha miradi kwa wakati, kuepuka uzembe katika usimamizi na kuhakikisha utunzaji wa vifaa hususan vya afya, ili kuongeza tija kwa wananchi.
“Serikali inajitahidi sana katika kampeni ya kupunguza vifo vya mama na mtoto, hivyo ni wajibu wetu kuunga mkono juhudi hizo kwa kujituma, kutimiza majukumu yetu na kutunza vifaa tulivyonavyo,” alisema Mnyema.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Mhe. Petro Magoti, amewataka watendaji kufanya kazi kwa bidii na kujituma hususan katika usimamizi wa miradi ya maendeleo, ili iwanufaishe wananchi na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukuza maendeleo ya Taifa.
Ameongeza kuwa kuanzia Jumamosi atarejea wilayani humo kufuatilia maendeleo ya miradi inayoendelea kukamilishwa pamoja na utekelezaji wa maelekezo yaliyotolewa na Katibu Tawala.
“Hatucheki na mtu kwenye miradi. Kuanzia Jumamosi nitakuwa hapa kuhakikisha mambo yote yaliyoanishwa yanatekelezwa,” alisema Mhe. Magoti.
Katika ziara hiyo, Katibu Tawala alikagua miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa soko la Kilindoni lenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 700, ujenzi wa jengo la wazazi katika Hospitali ya Wilaya lenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 500, pamoja na maboresho ya majengo ya Shule ya Msingi Utende yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 85.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.