Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Rashid Mchatta, amefunga rasmi Mashindano ya Michezo ya UMITASHUMTA ngazi ya mkoa, yaliyowakutanisha washiriki kutoka Halmashauri zote tisa (9) za Mkoa wa Pwani.
Mashindano hayo yalifanyika katika Viwanja vya Shirika la Elimu Kibaha, yakihusisha jumla ya wanafunzi 956 pamoja na walimu 71 waliowasindikiza na kuwaongoza wanamichezo hao.
Akizungumza wakati wa kufunga mashindano hayo, Mchatta aliwapongeza washiriki wote kwa juhudi, nidhamu na ushindani waliouonesha. Pia aliwashukuru walimu na waratibu wa michezo kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha mashindano hayo. Alisisitiza kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kuibua vipaji, kujenga afya na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa vijana.
“Mashindano haya yameonyesha vipaji vya hali ya juu, nidhamu na ushindani mzuri. Mkoa wa Pwani utaendelea kuyaendeleza mashindano haya kama njia ya kulea vipaji na kukuza afya kwa vijana wetu,” alisema Mchatta.
Kupitia mashindano hayo, wanamichezo 160 bora wameteuliwa kuingia kambini kwa ajili ya kuunda Timu ya Mkoa. Baada ya mazoezi na mchujo wa mwisho, wanamichezo 120 watachaguliwa kuiwakilisha Mkoa wa Pwani katika Mashindano ya Kitaifa ya UMITASHUMTA yatakayofanyika mkoani Iringa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.