Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema leo Julai 15, 2025, ameongoza kikao kazi na viongozi mbalimbali wa Mkoa huo kilicholenga kujitambulisha, kuimarisha mshikamano wa kiuongozi na kuweka msisitizo juu ya utekelezaji wa majukumu ya serikali kwa ufanisi na tija kwa wananchi.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani na kuhudhuriwa na Wakuu wa Sehemu na Vitengo kutoka Sekretarieti ya Mkoa, Makatibu Tawala wa Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa huo.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Katibu Tawala amesisitiza umuhimu wa kuongeza vyanzo vya mapato kwa kuendelea kubuni na kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo itakayochochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa.
“Niwapongeze kwa kazi nzuri mnayoifanya, hususan katika ukusanyaji wa mapato ambapo mmevuka malengo. Hata hivyo, Mkoa wa Pwani bado una nafasi kubwa ya kuongeza mapato zaidi kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato,” alisema Mnyema
Aidha, alisisitiza masuala ya uadilifu na uwajibikaji kwa watumishi wa umma, usimamizi madhubuti wa mapato ya ndani, utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa ufanisi, utoaji wa huduma bora kwa wananchi, ushirikiano wa kisekta, matumizi sahihi ya mifumo ya serikali pamoja na utunzaji wa rasilimali na miundombinu ya umma.
“Nisisitize pia umuhimu wa kuheshimiana, kupendana, kuhurumiana na kuweka mahusiano mazuri baina ya viongozi na watumishi, tukiwa wamoja na waadilifu, tutajenga msingi madhubuti wa utekelezaji wa mipango ya serikali kwa mafanikio zaidi,” aliongeza Mnyema.
Akizungumza Kwa niaba ya washiriki wa kikao hicho, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kibaha Regina Bieda alimshukuru Katibu Tawala kwa miongozo na maelekezo aliyoyatoa na akaahidi kuwa viongozi na watumishi wataendelea kuyatekeleza kwa bidii na uaminifu ili kuleta matokeo chanya kwa maendeleo ya Mkoa wa Pwani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.