Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, kampuni ya FARMBASE Ltd, na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) wameibuka vinara katika Maonesho ya Kilimo ya Nane Nane Kanda ya Mashariki 2025 yaliyofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere, Morogoro.
Kinondoni iliongoza kwa kishindo katika kundi la Halmashauri, FARMBASE Ltd ikang’ara kama mshindi bora upande wa kampuni za zana za kilimo, huku TARI ikionesha umahiri mkubwa katika kundi la taasisi za utafiti wa kilimo. Ushindi wa taasisi hizo umetokana na ubunifu wa hali ya juu, matumizi ya teknolojia rahisi na rafiki kwa wakulima, pamoja na uwezo wao wa kufikisha elimu ya kilimo kwa ufanisi kwa wakulima na wananchi waliotembelea mabanda yao.
Maonesho haya yaliyojumuisha jumla ya washiriki 138 kutoka mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Tanga, yalilenga kuhamasisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika kilimo na kutoa jukwaa la mafunzo kwa wakulima wadogo, vijana, wanawake na wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo.
Washiriki waligawanywa katika makundi 15 kulingana na asili ya taasisi zao, yakiwemo mashirika ya serikali, sekta binafsi, mashirika ya kimataifa, taasisi za fedha, na vyama vya wakulima. Kila kundi lilipimwa kwa kutumia vigezo mbalimbali vya kitaalamu ikiwemo ubora wa banda, ujumbe wa maudhui, na namna walivyoshirikisha makundi maalum kama vijana na wanawake.
Akikabidhi vikombe vya ushindi kwa taasisi zilizofanya vizuri, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Batilda Burian, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kilele cha maonesho hayo, aliwapongeza washiriki wote kwa kushiriki kikamilifu na kuonesha ubunifu mkubwa.
“Nimevutiwa sana na teknolojia zilizobuniwa na vijana, wanawake, na vikundi vya uzalishaji. Mbinu walizoonesha zimejikita katika kuongeza thamani ya mazao, kupunguza hasara baada ya kuvuna, na kuchochea kilimo biashara,” alisema Mhe. Burian.
Alitoa wito kwa washiriki wengine kuendelea kuboresha huduma na mawasilisho yao ili waweze kujipatia ushindi katika maonesho yajayo.
Maonesho ya mwaka huu yaliendeshwa chini ya kaulimbiu isemayo: “Chagua kiongozi boro kwa Maendeleo Endelevu ya kilimo, mifugo na Uvuvu"
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.