Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge, amelitaka Baraza la Biashara Mkoni humo kuandaa Mikakati Madhubuti ya Kukuza biashara na kuvutia wawekezaji katika kufursa mbalimbali zilizopo mkoani humo.
Kunenge ameyasema hayo leo Mei 13, 2024, wakati akifungua Mafunzo ya siku mbili ya uendeshaji na Majadiliano kati ya Sekta ya Umma na Binafsi katika Mkoa wa Pwani, yanayoratibiwa na Idara ya Uwezeshaji Kiuchumi na Maendeleo ya Sekta Binafsi, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu.
Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kutafuta wawekezaji kuja kuwekeza hapa nchini ambapo Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa Mikoa inayonufaika na jitihada hizo na kuwa ni wa kwanza kwa uwingi wa Viwanda nchini, hivyo akalitaka Baraza hilo kuunga mkono jitihada hizo kwa kuhakikisha mazingira ya Uwekezaji Mkoani Pwani yanaboreshwa.
“Ndugu zangu wana Pwani Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa na maono na miongozo mizuri ya namna ya kuliongoza vyema Taifa hili na kukuza uchumi wake kupitia sekta mbalimbali ikiwemo Viwanda, Biashara na Uwekezaji," amesema.
Ameliambia Baraza hilo kuwa linatakiwa kuzingatia vipaumbele vya Rais katika kukuza uchumi na kuongeza wawekezaji hapa nchini kwa kuwezesha mazingira mazuri ya biashara na uwekezaji.
“Mkoa wa Pwani, umejaaliwa kuwa na fursa za kipekee za kijiografia na rasilimali nyingi ambazo tukiweza kuzitumia vizuri kupitia mashirikiano ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma tutaweza kupiga hatua kubwa katika maendeleo ya kiuchumi," amesema.
“kwa muda mrefu Mkoa wa Pwani umekuwa mdau muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa Tanzania kupitia fursa za kijiografia na miundombinu wezeshi ikiwemo barabara, reli, umeme na maji. Fursa hizo zimeufanya Mkoa huu kuwa rahisi kufikika.” amebainisha Kunenge na akasema kuwa Mafunzo hayo yaende sambamba na majadiliano ya kimkakati ya kukuza ufanisi kwenye viwanda ili kutoa mchango wa Mkoa katika pato la Taifa.
Mkuu huyo wa Mkoa pia amezielekeza Taasisi wezeshi kuweka mazingira rafiki miundombinu yote muhimu inakuwepo, akitolea mfano Miondombinu ya Barabara, maji na Umeme ili kuendelea kuvutia uwekezaji mwingi katika mkoa huo huku akitahadharisha kuwa hayupo tayari kusikia kuna uwekezaji umeingia mkoani humo ukafa ama kufungwa na kuhamishwa kwenda nje ya eneo hilo akisema “ni mkakati gani ambao tunao kama Baraza la biashara la mkoa ili tujue kuwa sisi kama mkoa tunataka kwenda wapi," amesisitiza Kunenge.
Kwa Upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Uwezeshaji Kiuchumi na Maendeleo ya Sekta Binafsi Kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Conrad Milinga, Ameeleza kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuyajengea uwezo mabaraza ya biashara na kuwaleta pamoja wadau wa sekta binafsi na sekta ya umma ili kufanya kazi kwa Pamoja kama wabia.
Milinga amesema mabaraza hayo pia yanatakiwa kutambua kwamba sekta binafsi ndio inaendesha uchumi, kuongeza ajira na kuchakata na kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa ndani ya nchi ili kuweza kuongeza mapato ya Serikali. na kuwa sekta hizo kwa pamoja ni wadau wakuu wa serikali hivyo ni lazima watambuane na kushirikiana.
Amesema kumekuwa na pengo kubwa kati ya ushirikiano wa kimajukumu kati ya sekta binafsi na za umma jambo hilo sasa linakwenda kuondolewa kupitia majadiliano ambapo kila mmoja atapata nafasi ya kuzungumza na kueleza changamoto zilizopo na namna ya kuzitatua.
Akitoa mada kwenye mafunzo hayo, Afisa Mkuu wa Uchumi, biashara na uwekezaji Mwamini Nkwizu amesema mabaraza ya biashara nchini yamefanya kazi kubwa kuongeza na kuchochea tija katika masuala mengi ambayo yalikuwa na ukinzani japo pia aliyataka kutengeneza ajenda za pamoja kama mkakati wa kuondokana na changamoto zilizopo.
Amesema maeneo mengi yaliyofanyiwa utafiti na tathmini iliyotolewa na ofisi ya taifa ya Takwimu NBS inaonesha kuwa mkoa wa Pwani umefanya vizuri katika kusimamia mabaraza hayo kwa kushika nafasi ya pili hususani pia katika kuweka manegementi nzuri kwa kuwasiamia wafanyabiashara ndogondogo maarufu kama "machinga."
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.