Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, ameomba kuundwa kwa timu maalum ili kusimamia urejeshaji wa huduma ya vivuko vya MV Kilindoni na Meli ya TSN Songosongo vinavyotoa huduma ya usafiri kati ya Nyamisati, Wilaya ya Rufiji, na Mafia, baada ya huduma hiyo kusimama tangu Oktoba 10 mwaka huu. Kunenge alitoa ombi hilo leo akiwa katika ziara ya ukaguzi na uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Mafia, akiwa ameambatana na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa.
Kunenge alitoa wito huo katika ofisi ya Wilaya ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Mafia, akiomba timu ya watu watakaosimamia urejeshaji wa huduma hizo muhimu.
Baada ya kupokea ombi hilo, Waziri Bashungwa, akiwa katika ukaguzi wa matengenezo ya Meli ya TSN Songosongo yanayosimamiwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, aliagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi kuunda timu itakayojumuisha Ofisi ya RAS Pwani, Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi, TEMESA, JWTZ, na wadau wengine ili kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto ya vivuko wilayani Mafia.
Hatua hii imechukuliwa baada ya vivuko vya MV Kilindoni na Meli ya TSN Songosongo kuharibika, hali iliyosababisha kukwama kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi wilayani humo.
Bashungwa alieleza kuwa serikali inatambua umuhimu wa huduma za usafiri wa vivuko katika Wilaya ya Mafia, na imechukua juhudi za kuhakikisha vivuko vyote viwili vinapatikana ili endapo kimoja kiharibike, kingine kiweze kuendelea kutoa huduma. Aliongeza kuwa serikali ina mpango wa kuongeza kivuko kingine ili kuimarisha huduma hizo.
“Serikali imechukua jitihada za haraka na makusudi, pamoja na timu hii kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, ili kurudisha huduma ya vivuko viwili,” alisema Mhe. Bashungwa.
Aidha, Waziri Bashungwa akiwa wilayani humo ameweka jiwe la msingi katika Zahanati ya Kilindoni yenye gharama ya milioni 190 kutoka Serikali Kuu, pamoja na Shule ya Sekondari ya Raphta yenye thamani ya zaidi ya milioni 500.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.