Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, amefanya ziara ya kikazi katika kiwanda cha kuunganisha magari aina ya FAW cha Kampuni ya Rostar Vehicle Equipment Limited kilichopo wilayani Bagamoyo, ambapo alipata fursa ya kukagua Ujenzi wa kiwanda na kujionea magari mbalimbali yaliyokwisha kuunganishwa, hususan ya aina ya Tipper na kupokea taarifa ya Mradi.
Katika ziara hiyo, Mhe. Kunenge alieleza kuridhishwa kwake na namna wawekezaji wa kiwanda hicho walivyoshirikisha vijana wa Kitanzania katika shughuli za uundaji wa magari, akisisitiza kuwa vijana hao wana uwezo mkubwa na ubunifu wa hali ya juu.
“Vijana wapo na wana uwezo mkubwa wa kufanya shughuli hizi. Ni wafanyakazi wabunifu na wenye juhudi. Nawapongeza sana,” alisema Mhe. Kunenge.
Aidha, aliwashukuru wawekezaji kwa kuamua kuwekeza wilayani Bagamoyo na kusisitiza kuwa uwekezaji huo ni mkubwa na muhimu kwa maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.
“Hiki ni kiwanda kikubwa cha kuunganisha magari ya FAW barani Afrika, nawapongeza sana kwa maono haya makubwa,” aliongeza Kunenge.
Pia aliwapongeza kwa kuwa waaminifu katika ulipaji wa kodi, jambo alilosema linaonesha uzalendo na uelewa wa wajibu wao kwa taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa kiwanda hicho, Bw. Bai Xinguo, alisema ujenzi wa kiwanda hicho ulianza mwezi Juni 2024 na sasa umekamilika kwa awamu ya kwanza ambapo tayari kimeanza uzalishaji wa magari. Kiwanda hicho kinategemea kuzalisha magari, trailer za magari, tank, Pamoja na cranes
Bw. Xinguo alieleza kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha magari 500,000 kwa mwaka na tayari wamepokea oda ya magari 1000 kutoka kwa wateja mbalimbali.
Aidha, alitoa shukrani kwa serikali kwa usaidizi katika hatua mbalimbali za kuanzisha kiwanda hicho, huku akiomba msaada zaidi katika ujenzi wa barabara ya kufika kiwandani hapo.
Katika kujibu ombi hilo, Mhe. Kunenge aliahidi kuwa serikali ya mkoa italifanyia kazi suala hilo kwa kushirikiana na mamlaka husika ili kuhakikisha miundombinu ya kufika kiwandani inaboreshwa.
Katika hatua nyingine Mhe Kunenge amemuagiza Mkurugenzi wa Halmshauri ya Wilaya ya Bagamoyo kuanza kupanga Mji eneo Hilo na watu wote wanaomiliki Ardhi eneo Hilo wafuate ramani ya mipango miji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.