Leo Julai 15, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ulioongozwa na Mkuu wa Biashara wa Benki hiyo, Bw. Moses Minja.
Ujumbe huo umetembelea ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa lengo la kuonesha nia ya kuimarisha ushirikiano kati ya NBC na Serikali ya Mkoa wa Pwani, hususan katika masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwemo huduma za kifedha.
Akizungumza kwa niaba ya ujumbe wake, Bw. Minja ameipongeza Serikali ya Mkoa wa Pwani kwa jitihada mbalimbali za maendeleo zinazotekelezwa katika mkoa huo. Aidha, alieleza dhamira ya NBC kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuchangia maendeleo ya wananchi kupitia huduma za kifedha na miradi ya kijamii.
“Tupo tayari kushirikiana nanyi katika maeneo mbalimbali ya maendeleo, na tutaendelea kutoa mchango wetu pale tutakapohitajika,” alisema Minja.
Kwa upande wake, Mhe. Kunenge ameishukuru Benki ya NBC kwa utayari wake wa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Pwani, huku akieleza kuwa benki hiyo imekuwa mdau muhimu katika maendeleo ya mkoa.
“Napenda kuwasisitiza kuwa Serikali ya Mkoa ipo pamoja nanyi. Tuna mambo mengi ya kushirikiana, hivyo tunawaomba mzidi kutupatia ushirikiano pale tunapowahitaji,” alisema Mhe. Kunenge.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.