Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, ametoa wito kwa watumishi wa umma kuwa na mshikamano, uwajibikaji, upendo na kuheshimiana ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya serikali kwa manufaa ya wananchi.
Akizungumza na watumishi wa ofisi ya mkoa leo, Mnyema aliwasisitiza kuzingatia maadili ya utumishi wa umma, huku akiwataka kuishi karibu na vituo vya kazi ili waweze kufahamu changamoto halisi za wananchi na kuzitafutia suluhisho kwa wakati.
“Kubwa ninaloliomba kwenu ni ushirikiano, upendo na uwajibikaji. Nifanye sehemu yenu katika safari hii ya kulitumikia taifa,” alisema Mnyema.
Aidha, alikumbusha kuwa kila mtumishi ana jukumu kubwa la kuhakikisha serikali inatimiza ahadi zake kwa wananchi, na kwamba mafanikio yatapatikana iwapo kutakuwa na mshikamano na heshima kwa kila mmoja.
“Tutambue kuwa kila mmoja wetu ana dhamana katika kutekeleza majukumu ya serikali. Tukishirikiana kwa dhati bila mtu kujiona bora kuliko mwenzake, tutaweza kufanikisha malengo yetu,” aliongeza.
Kwa niaba ya watumishi, Mkuu wa Kitengo cha Ukaguzi, Obadia Malima, alimshukuru Katibu Tawala huyo kwa maelekezo yake na kuahidi kuwa watayatekeleza kikamilifu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.