Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Nsajigwa George, ameongoza uzinduzi wa kampeni ya ugawaji wa vyandarua zaidi ya 971,000 bure kwa kaya 426,637 mkoani Pwani, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutokomeza ugonjwa wa malaria ifikapo mwaka 2030.
Uzinduzi huo umefanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kibaha, na kuhudhuriwa na wawakilishi kutoka TAMISEMI wakiongozwa na Mratibu wa Malaria Taifa, Stella Kanyange, pamoja na Peter Gitanya, Afisa Mkuu wa Afya kutoka Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria (NMCP) chini ya Wizara ya Afya. Pia walikuwepo wajumbe wa Kamati ya Usalama, Wakuu wa Sehemu na Vitengo kutoka Sekretarieti ya Mkoa, Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Kusirye Ukio, viongozi wa dini na wadau mbalimbali wa afya.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Nsajigwa alieleza kuwa kampeni hiyo itaanza rasmi kutekelezwa kuanzia Agosti 15, 2025, katika kata 108 na vijiji/mitaa 426, ambapo zaidi ya watu 1,633,774 wanatarajiwa kunufaika na vyandarua hivyo vinavyotolewa bure.
Aidha, alibainisha kuwa Mkoa wa Pwani umeendelea kupiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya malaria, ambapo kiwango cha maambukizi kimeteremka kutoka asilimia 15.3 mwaka 2016 hadi asilimia 6.7 mwaka 2022.
“Idadi ya vifo vitokanavyo na malaria imepungua kwa asilimia 27 kutoka vifo 110 hadi 30. Hii ni hatua kubwa ya mafanikio katika mkoa wetu, na ni matokeo ya matumizi sahihi ya vyandarua, unyunyiziaji wa dawa, na usafi wa mazingira,” alisisitiza Nsajigwa.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt. Kusirye Ukio, alisema Mkoa tayari umeanza kampeni ya uhamasishaji kutoka wilaya hadi vijijini ili kuondoa kabisa ugonjwa wa malaria.
Aliongeza kuwa Mkoa umepokea lita 24,000 za dawa maalum kwa ajili ya kuua viluwiluwi vya mbu, ambazo zitatumika kudhibiti mazalia katika maeneo mbalimbali.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Idara ya Afya – Ofisi ya Rais TAMISEMI, Stella Kanyange alisema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inajivunia mafanikio makubwa ya kupunguza maambukizi ya malaria kutoka wastani wa asilimia 15 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 8.1 mwaka 2022.
“Mapambano dhidi ya malaria yanahitaji ushirikiano wa kila mmoja wetu. Kauli mbiu yetu ni Mimi, Wewe, na Tanzania Bila Malaria ifikapo 2030 – Inawezekana,” alisema Kanyange.
Kampeni hii inaratibiwa kwa pamoja na Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Bohari ya Dawa (MSD), pamoja na Mfuko wa Dunia wa Kupambana na Magonjwa ya Malaria, Kifua Kikuu na UKIMWI (Global Fund). Lengo kuu ni kuokoa maisha na kujenga jamii yenye afya bora isiyo na malaria.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.