Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Pili Mnyema, ameanza ziara ya kikazi katika Halmashauri zote za Mkoa huo kutembelea, kukagua miradi ya maendeleo na kuongea na watumishi.
Katika ziara hiyo iliyoanza leo Agosti 12, 2025 kwa kuitembelea Manispaa ya Kibaha, Mnyema amesisitiza umuhimu wa ubunifu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuongeza mapato ya Halmashauri pamoja na Mkoa kwa ujumla.
"Naomba tumuunge mkono Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kubuni vyanzo vipya vya mapato. Hili ni miongoni mwa maagizo niliyopatiwa ili kusaidia kuongeza mapato ya Mkoa wetu," alisema Mnyema.
Aidha, alimpongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, kwa kuendelea kubuni na kusimamia miradi mbalimbali yenye tija, ambayo imesababisha ongezeko la mapato ya Manispaa hiyo kila mwaka.
Mnyema aliwataka watumishi wa Manispaa hiyo kuendelea kufanya kazi kwa kuzingatia misingi ya utumishi wa umma kwa kuwa na nidhamu, uadilifu, na bidii ili kutoa huduma bora kwa wananchi ambapo alisisitiza pia umuhimu wa uwajibikaji na uaminifu katika usimamizi wa fedha za umma, ili kudhibiti upotevu wa rasilimali na kuongeza ufanisi katika miradi ya maendeleo.
Akiwa katika Manispaa hiyo, Katibu Tawala huyo alitembelea na kukagua miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Mchepuo wa Kiingereza – Mwalimu Nyerere iliyopo Kata ya Sofu, pamoja na mradi wa maduka ya biashara ya uitwwo "Kibaha Shopping Mall."
Ziara hiyo inalenga kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kufanya vikao kazi na watumishi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Pwani na Kesho anatarajiwa kuendelea na ziara hiyo kwa kutembelea Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.