Serikali ya Tanzania, kupitia Mpango wa TASAF (Tanzania Social Action Fund), kwa kushirikiana na UNICEF, imezindua rasmi Programu ya Stawisha Maisha katika kijiji cha Mkiu, kata ya Mkamba, wilaya ya Mkuranga. Uzinduzi huu ulifanyika tarehe 29 Oktoba 2024, na unalenga kuboresha lishe kwa watoto wenye umri wa miaka 0 hadi 5, wanawake wajawazito, na mabinti balehe kwa kuwapatia elimu kuhusu lishe bora kupitia vipindi vya redio.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Shedrack Mziray, alieleza kuwa mradi huu ni sehemu ya juhudi za kupunguza utapiamlo katika kaya zinazohusishwa na mpango wa TASAF. "Kupitia mpango huu, tutakuza rasilimali watu na kuwezesha kaya kujinasua kutoka kwenye umaskini kwa kuzingatia elimu ya lishe bora watakayopatiwa," alisema Mziray.
Aidha, aliongeza kuwa redio zinazotumia nishati ya jua zitatumika kuwahamasisha wanajamii kushiriki mijadala kuhusu lishe bora na kutoa elimu na burudani. Kipindi hiki kitatolewa mara moja kwa wiki kwa kipindi cha miezi sita.
Akiongea kwa niaba ya uongozi wa Mkoa wa Pwani, Mratibu wa TASAF Mkoa Roseline Kimaro alisisitiza kuwa serikali ya mkoa inaendelea kuimarisha uchumi wa kaya za wanufaika kupitia mpango wa TASAF kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo, ikiwemo UNICEF. Kimaro alieleza kuwa mkoa unatekeleza mikakati iliyowekwa na serikali ili kuboresha lishe na kupunguza utapiamlo unaosababisha udumavu kwa watoto.
Nae katibu Tawala wa Wilaya ya Mkuranga, kwa upande wake Omary Mwanga, alitoa shukrani kwa TASAF na UNICEF kwa mchango wao katika mpango wa lishe bora. Pia Pia aliwahamasisha wananchi wa wilaya ya Mkuranga kushiriki kikamilifu katika mpango huu ili kuleta matokeo chanya katika kaya zao na kujikinga dhidi ya udumavu. "Serikali imewekeza kwa ajili yetu, hivyo tuhakikishe tunapata thamani ya vifaa na elimu tunayopata," alisema Mwanga.
Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga ni miongoni mwa halmashauri 18 zilizochaguliwa kutekeleza mpango huu wa majaribio wa Stawisha Maisha. Katika utekelezaji huu, vikundi 30 vimeundwa katika kata 13 na vijiji 19, ambapo wanakutana mara moja kwa wiki kusikiliza vipindi vya redio vyenye maudhui ya lishe bora na afya kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.