MAKAMU mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara ,Philip Mangula ameitaka bohari ya madawa (MSD) ,kuangalia namna ya kununua dawa ya viuadudu vya mazalia ya mbu,inayotengenezwa na kiwanda cha Biotech kilichopo Kibaha mkoani Pwani ili kuzuia malaria badala ya kupoteza mamilioni ya fedha kununua madawa kutoka nje kwa ajili ya kutibu ugonjwa huo.
Aidha ameitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na Halmashauri zote nchini kununua bidhaa hiyo ili kutatua changamoto ya ukosefu wa soko iliyopo kiwandani hapo.
Pamoja na hayo,Mangula amekielekeza kiwanda hicho kujitangaza ndani na nje ya nchi ,ili kuitangaza bidhaa wanayozalisha na kueleza manufaa yake .
Ushauri huo aliotoa wakati alipotembelea kiwanda hicho cha Bioteh Products Ltd Kibaha, kabla ya safari yake ya siku kumi nchini Cuba ambako amealikwa na Chama Cha Kikomunist nchini humo.
Mangula alisema gharama zinazotumika kutibu ni kubwa kuliko zinazotumika kuzuia hivyo haina budi kuzuia kabla ya tiba.
Aidha alieleza kuwa halmashauri zote nchini, MSD pamoja na Wizara ya Afya zina wajibu wa kushirikiana kununua dawa hizo ili kutatua changamoto ya soko iliyopo.
“Tunahitaji elimu na kujitangaza zaidi juu ya umuhimu wa dawa hii,ili
kuzuia malaria”alisema Mangula.
Hata hivyo ,Mangula alielezea kuwa,kuna viwanda vinne duniani vinavyozalisha dawa ya viuadudu vya mazalia ya mbu ikiwemo Japan ,Marekani ,Cuba na Tanzania hivyo anaamini kinachofanyika Japan ndiokinachofanyika kiwandani hapo .
“Nimepata mwaliko wa kwenda Cuba natarajia kuondoka na mrejesho wa namna kiwanda kinavyoendelea ili niwe na la kujibu kama itatokea kuulizwa lolote juu ya maendeleo ya kiwanda,
“Katika safari hii moja ya eneo nitakalopitia katika safari yangu ni pamoja na kiwanda cha aina hii nchini humo,nimeona itakuwa ni aibu nisije kwenda huko ikatokea kuulizwa lolote nikakosa la kujibu”alisisitiza Mangula.
Mangula alisema, kiwanda kinatakiwa kuzalisha lita mil.sita kwa mwaka, lakini kimeshazalisha lita zaidi ya 400,000 pekee kwa miaka miwili kutokana na kukosa soko la uhakika
“Tunaelezwa viuadudu hivi vinazalishwa na kuwa na uwezo wa kukaa kwa miaka miwili dawa inatakiwa kumwagwa hivyo huwezi kuzalisha kiwango kikubwa wakati soko hakuna “.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Pwani ,Mhandisi Evarist Ndikilo ,alisema tatizo la soko bado ni tatizo.
Alisema katika Mkoa wa Pwani watu 720,000 waliugua ugonjwa wa malaria ndani ya miaka mitatu iliyopita ambapo vifo vilivyotokana na ugonjwa huo ni 280 hali inayoonyesha ugonjwa huo bado ni tishio kimkoa.
Mhandisi Ndikilo alisema kuwa,Mkoa wa Pwani unatekeleza agizo la serikali na ilani ya Chama Cha Mapinduzi ambapo kwasasa ina zaidi ya viwanda 400 vikubwa ,vya kati na vidogo .
Kwa upande wake, meneja wa udhibiti wa ubora na viwango kiwandani hapo , Samwel Mziray , alisema mteja mkuu wa ndani wa bidhaa hiyo ni Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambayo NDC imeingia mkataba nayo wa kuuza biolarvicides na wizara hiyo kwa mpaka sasa haijaanza kuutumia.
Alitaja changamoto kubwa pia ni madeni kwa halmashauri mbalimbali ambazo zinadaiwa bilioni 1.7 hadi sasa .
Mziray alibainisha kwamba, tatizo jingine ni ucheleweshaji wa malipo kutoka serikalini na soko
Alieleza ,kiwanda bado kina kiasi kidogo cha lita 5,920 zenye gharama ya milioni 78.144.
Kiwanda hicho kiliwekwa jiwe la msingi na Rais mstaafu Jakaya Kikwete oktoba 2013 na kufunguliwa rasmi Julai 2015 ambapo kimegharimu dollar za kimarekani milioni 22 na ajira 110.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.