Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dk. Kusirye Ukio, ameishukuru Benki ya Stanbic Tanzania kwa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi milioni 60, uliotolewa kwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani (Tumbi), akisema msaada huo utapunguza changamoto ya upungufu wa vifaa katika utoaji huduma za afya.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano yaliyofanyika hospitalini hapo leo, Oktoba 11, 2025, Dk. Ukio alisema vifaa hivyo vitasaidia kuongeza ufanisi wa huduma na kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa afya.
“Tumbi inapokea mamia ya wagonjwa kila siku kutoka mikoa jirani kama Morogoro, Dar es Salaam na Lindi, hivyo msaada huu unaleta ahueni na matumaini mapya kwa wagonjwa na watumishi wetu,” alisema Dk. Ukio.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na kompyuta, vitanda, viti vya wagonjwa (wheelchairs), matoroli na vifaa vya usafi, ambavyo vitatumika katika idara mbalimbali zenye wingi wa wagonjwa kila siku.
Msaada huo ulikabidhiwa na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi na Wateja Maalumu wa Stanbic Bank, Omari Ntiga, kwa niaba ya benki hiyo, ambapo alisema kuwa ni sehemu ya mpango wa benki kusaidia jamii kupitia miradi endelevu inayogusa sekta muhimu kama afya, elimu na mazingira.
“Tunatambua sekta ya afya ni uti wa mgongo wa ustawi wa jamii. Tunataka wagonjwa wapate huduma bora na watumishi wafanye kazi katika mazingira bora yenye vifaa vya kisasa,” alisema Ntiga.
Baadhi ya wananchi waliokuwepo wakati wa tukio hilo, akiwemo Kulwa Yohana na Christina Mabawa, walipongeza hatua ya Stanbic Bank, wakisema taasisi binafsi zina nafasi kubwa katika kuboresha huduma za kijamii kupitia ushirikiano na serikali.
“Tunaona si kila kitu lazima kifanywe na Serikali. Msaada kama huu unagusa maisha ya watu moja kwa moja,” alisema Christina.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na watumishi wa hospitali, viongozi wa serikali za mitaa na wawakilishi wa Stanbic Bank kutoka matawi mbalimbali ya mkoa wa Pwani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.