Maliasili na Utalii
Mkoa wa Pwani una jumla ya Misitu 99 yenye eneo la hekta 542,591.4 kati ya hiyo, Misitu 30 yenye eneo la hekta 222,228 ipo chini ya usimamizi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS); Misitu 15 yenye eneo la hekta 88,960.6 ipo chini ya usimamizi wa Halmashauri na Misitu 52 yenye eneo la hekta 231,402.8 ipo chini ya usimamizi wa Serikali za Vijiji na Misitu miwili (2) ni ya Hifadhi ya Mazingira Asilia ambayo ni Pugu Kazimzumbwi na Uzigua.
Mkoa wa Pwani una jumla ya vivutio vya utalii 87 vinavyojumuisha Mambokale, Misitu ya Hifadhi ya Mazingira Asilia, Mapori ya Akiba, Hifadhi za Taifa na Fukwe za bahari. Vivutio hivi vinasimamiwa na Taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) na Hifadhi ya Bahari Mafia (HIBAMA).
Sekta ya Wanyamapori inajumuisha Hifadhi za Jumuiya za Wanyamapori ‘Wildlife Management Areas – WMAs’ za Juhiwangumwa na Mungata zilizoko Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji, Mapori ya Akiba ya Selous na Wami-Mbiki, Hifadhi za Taifa za Nyerere na Saadani ambazo hutumika kwa ajili ya Utalii wa Wanyamapori na Picha. Saadani ni kati ya Hifadhi chache Ulimwenguni zinazopakana na Bahari na zinazohifadhi Mazalia ya Kasa wa Kijani ‘Green Turtles’. Licha ya kutunza Bioanuai, Pori la Akiba la Selous na Hifadhi ya Saadani zimesaidia huduma za kijamii kwa Vijiji vinavyozunguka katika Wilaya za Rufiji, Kisarawe na Bagamoyo kwa kuingiza asilimia 25 ya mapato yanayotokana na Uwindaji wa Kitalii kwenye Vijiji hivyo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.