Wananchi wa Kijiji cha Minazi Mikinda wilayani Kibaha wamefurahia kukamilika kwa ujenzi na usajili wa Shule ya Sekondari Mwakamo-Ruvu, wakisema mradi huo ni mkombozi mkubwa kwa watoto wao na utachangia kuinua elimu pamoja na kuwapatia vijana ujuzi wa kujitegemea.
Wamesema shule hiyo itawaondolea wanafunzi adha ya kutembea umbali mrefu kufuata elimu ya sekondari, sambamba na kuwapa fursa ya kujifunza fursa za ufundi na stadi za maisha, zinazowaandaa kukabiliana na changamoto za ajira.
“Tumeipokea kwa furaha kubwa shule hii. Itasaidia watoto wetu wasome karibu na nyumbani na kupata elimu yenye ujuzi wa kujiajiri,” alisema mmoja wa wananchi, Asha Mkwizu, mkazi wa kijiji hicho.
Ujenzi wa shule hiyo umetekelezwa na Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha kupitia Divisheni ya Elimu Sekondari, kwa gharama ya shilingi milioni 528.9 zilizotolewa na Serikali Kuu. Shule hiyo inalenga kutoa elimu ya sekondari yenye mwelekeo wa ujuzi mashinani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, Regina Bieda, amesema mradi huo ni sehemu ya jitihada za Serikali katika kuinua kiwango cha elimu na kuandaa wanafunzi wenye stadi zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira.
“Shule hii ya Mwakamo-Ruvu siyo tu kwamba itarahisisha upatikanaji wa elimu ya sekondari, bali pia itawaandaa wanafunzi wetu kupata ujuzi wa ufundi utakao wawezesha kujitegemea na kuchangia maendeleo ya taifa,” alisema, Bieda.
Kwa upande wake, Afisa Elimu Sekondari wa Wilaya ya Kibaha, Khadija Rajab, amesema shule hiyo inatarajiwa kuanza kupokea wanafunzi mwanzo wa mwaka 2026, na maandalizi ya walimu pamoja na vifaa vya kufundishia yanaendelea.
Mradi huu unatajwa kuwa sehemu ya utekelezaji wa dira ya kitaifa ya elimu bora, jumuishi na yenye mwelekeo wa stadi za maisha, hatua inayotarajiwa kuleta mapinduzi chanya katika elimu ya vijijini na kuchochea maendeleo ya jamii kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.