Mkuu wa mkoani Pwani, mhe. Abubakar Kunenge ameiagiza wilaya ya Mkuranga kusimamia mipango mji kwa kutenga maeneo ya viwanda hatua itakayosaidia kuondoa migogoro ya ardhi kati ya wananchi na wawekezaji wa viwanda.
Aidha amezielekeza Taasisi wezeshi kuondoa ukiritimba kwa wawekezaji badala yake watumie nafasi zao kuwaelekeza taratibu zinazotakiwa ili kufikia malengo waliyowekwa.
Kunenge alitoa maagizo hayo wakati alipotembelea kiwanda cha Vioo KEDA Tanzania, kata ya Mbezi, Mkuranga mkoani Pwani, ambacho hadi kukamilika kitagharimu fedha ya kimarekani 309,000,000usd ikiwa ni sawa na fedha ya kitanzania sh.bilioni 803.4.
Kunenge alisema, Serikali inaendelea kushirikiana na wawekezaji ili kuinua uchumi wa mkoa na Taifa kijumla.
Alifafanua, uwepo wa viwanda utasaidia ongezeko la ajira, kuongeza pato la Taifa sanjali na kukuza sekta ya viwanda nchini.
Vilevile Kunenge amejinasibu kuwa ongezeko la viwanda mkoani humo litaongeza uzalishaji wa bidhaa na malighafi hali itakayosaidia kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo nje ya nchi.
Alitaja mkoa una viwanda 1,535 kwasasa ambapo kati ya hivyo vikubwa ni 124.
Awali akitoa taarifa ya mradi, Ofisa biashara Ruby Zhu alisema, ujenzi wa mradi ulianza march 2023, mradi upo awamu kwanza ambapo utakamilika baada ya miezi 18 na awamu ya pili itaanza mwaka 2027.
"Wiki mbili ijayo tutafanya majaribio ya mashine na kupata gesi, na mwezi wa tisa wataanza uzalishaji ambapo kila siku watazalisha tani 600 na kwa mwaka watakuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni 219." alisema Ruby.
Ruby alieleza, wanatarajia kuwa na ajira zaidi 1,600, walianza uwekezaji mkoani Pwani kwa kuwekeza kiwanda cha marumaru Chalinze, Kiwanda cha taulo za watoto,sabuni KEDS Kibaha Mjini na Kiwanda cha Vioo Mkuranga.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.