Makamu wa Rais mama Samia Suluhu Hassan amesema Serikali haitamvumilia mtu atakayekwamisha ujenzi wa viwanda pamoja na kuingiza bidhaa feki hapa nchini.
Akizindua maonyesho ya bidhaa za Viwanda zinazozalishwa Mkoani Pwani Naibu Waziri Wizara ya Viwanda , Biashara Uwekezaji Mhe.Stella Manyanya kwa niaba ya Makamu wa Rais alisema kuwa, hakuna sababu ya kuweka vizuizi ambavyo vina namna ya kuvikabili katika kipindi hiki cha uchumi wa Viwanda.
Alisema pia, kitendo cha kuingiza bidhaa feki ni moja ya sababu zinazochangia kupoteza mapato ya nchi lakini pia kukosesha bidhaa bora zinazozalishwa hapa nchini.
Aidha kwa upande wake Naibu Waziri Manyanya alisema," Taasisi zinazohusika na udhibiti wa bidhaa hawana nafasi ya kusingizia sheria na kuleta usumbufu kwa wawekezaji".
Nae Mkuu wa Mkoa wa Pwani mhe. Mhandisi Evarist Ndikilo aliwapongeza wamiliki wa viwanda ambao wamekubali kushiriki katika maonyesho hayo kutangaza bidhaa zao.
Mhandisi Ndikilo alisema, maonyesho hayo ni moja ya jukwaa la kutangaza biashara zinazozalishwa katika Mkoa wa Pwani na kupata masoko.
Aidha alisema kuwa,maonyesho ambayo yalifanyika kwa Mara ya kwanza mwaka 2018 yamekuwa na mafanikio makubwa kwani tayari watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Pwani wamekuwa wanunuzi wakubwa wa bidhaa zinazizalishwa Pwani.
“Katika uongozi wa awamu ya tano unaosisitiza uwekezajj kwenye viwanda viwanda 300 vimejengwa na kuwezesha ajira 20,000 za moja kwa moja na 40,000 zisizo rasmi,”alisema Ndikilo.
Pia aliendelea kusema kuwa ,” mbali ya mafanikio ya ujenzi wa viwanda katika Mkoa huo, pia wanakabiliana na changamoto mbalimbali kutoka kwa baadhi ya wawekezaji kutumia vifaa duni sehemu za kazi”.
Changamoto nyingine ni, baadhi ya wamiliki wa viwanda kutofuata taratibu za kazi, kwa kutokuwa na mikataba kwa wafanyakazi wao, na malipo duni kwa wafanyakazi.
Mhandisi Ndikilo alisema,” kuna chagamoto kutoka kwa Taasisi wezeshi, na wamiliki wa viwanda ikiwemo kutoa adhabu kwa wamiliki, bila kutoa elimu na sababu za adhabu”.
Mkurugenzi wa TanTrade Edwin Rutageruka alitoa wito kwa wamiliki wa Viwanda kwenda kwenye masoko ya nje ya nchi ambako bidhaa za ndani zinauzika huko.
Alisema, wenye viwanda, wanatakiwa kushiriki kwenye masoko yaliyo nje ya Tanzania huku wakiwa na bidhaa zao bora ambazo zitafungua masoko zaidi.
Maonyesho hayo yanafanyika kwa Mara ya pili mfululizo yakifadhiliwa Makampuni mbalimbali ikiwemo benki ya CRDB, Kampuni ya TANGA SEMENT, Benki ya NMB,TIC,Lake Oil, TanTrade, TIB na wengine.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.