Serikali Mkoani Pwani imetoa eneo lenye ukubwa wa ekari 1000 ili lipimwe viwanja na kugawiwa kwa wakazi wanaoishi kwenye eneo oevu kwenye kitongoji cha Kisabi Mlandizi Wilaya ya Kibaha.
Hayo yamebainishwa leo Machi 12, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Simon aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge kwenye mkutano wa kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Mkuu huyo wa wilaya amefafanua kuwa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira - NEMC lilihadharisha juu ya eneo hilo kutumika kujengwa makazi ya binadamu kwa kuwa ni owevu linaloweza kusababisha madhara yatokanayo na mafuriko kikiwa ni pamoja na uwezekano wa nyumba kutitia.
Kutokana na hali hiyo, ofisi yake iliamua kutafuta eneo rafiki linalofaa kwa makazi ya binadamu ambalo ameeleza kuwa limepatikana katika Kijiji cha Kikongo na sasa maandalizi ya upimaji unaendelea ili wakazi hao wapewe viwanja.
Kwa upande wao, wakazi hao wa Kisabi wameiomba Serikali kuwaacha waendelee kuishi katika eneo hilo ambapo Mkuu wa Wilaya ameahidi kuyafikisha maombi hayo sehemu husika kwa lengo la kutoa maamuzi zaidi ingawa amesisitiza kuwa kutokana na ushauri wa kitaalamu kimazingira, eneo hilo si rafiki kwa makazi hivyo wananchi wanapaswa kuhama.
Katika hatua nyingine, awali, kwenye mkutano uliofanyika Picha ya Ndege Kibaha Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Simon ameahidi kushughulikia kero ya maji machafu yanayotiririka kutoka kwenye kiwanda cha Keds kilichopo Picha ya Ndege Halmashauri ya mji wa Kibaha.
Kero hiyoa imebainishwa na wakazi wa eneo hilo waliohudhuria kwenye mkutano ulioandaliwa na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani ili kusikiliza na kutatua kero za wananchi.
Akizungumza katika mkutano huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Simon amesema Serikali itashughulikia kero hiyo sambamba na kukutana na uongozi wa Kiwanda.
Katika mkutano huo pia Wananchi walieleza kero ya maji kwenye Mtaa wa Lulanzi ambapo Meneja wa Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salam (DAWASA) Kibaha Alfa Ambokile ameeleza kwamba utekelezaji wa utatuzi wake utaanza hivi karibuni.
Ambokile amesema upo mradi wa maji Pangani unatarajia kuanza utekelezaji wake hivi karibuni mradi ambao utafikisha maji katika eneo hilo la Lulanzi na ilipo Hospitali ya Wilaya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.