Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeendesha mafunzo ya siku mbili, Februari 2-3, 2025, kuhusu uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Pwani. Mafunzo hayo yanayofanyika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kibaha, yanawahusisha maafisa waandikishaji, maafisa waandikishaji wasaidizi wa ngazi ya jimbo, maafisa uchaguzi, maafisa ugavi, na maafisa TEHAMA wa halmashauri.
Akifungua mafunzo hayo, Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji wa Rufaa Mbarouk S. Mbarouk, alisema kuwa lengo la mafunzo ni kuwajengea maafisa waandikishaji ujuzi wa kutosha ili kuhakikisha uboreshaji wa daftari unafanyika kwa ufanisi. Pia, mafunzo haya yatawapa weledi katika ujazaji wa fomu na matumizi ya Mfumo wa Kuandikisha Wapiga Kura (Voters Registration System – VRS), ili kuwawezesha kutumia kwa ufasaha mfumo huo pamoja na vifaa vingine vya kuandikisha wapiga kura.
Mafunzo haya yatawawezesha maafisa hawa kuwafundisha waandikishaji wasaidizi wa ngazi ya kata, ambao nao baadaye watawafundisha waendeshaji wa vifaa vya biometriki pamoja na waandishi wasaidizi, ambao ndio watakaosimamia uandikishaji wa wapiga kura vituoni,†alisema Jaji Mbarouk.
Kwa upande wa maafisa TEHAMA, mafunzo haya yanawalenga kuwapa mbinu za kukabiliana na changamoto za kiufundi zitakazoweza kujitokeza wakati wa uandikishaji wa wapiga kura.
Aidha, Jaji Mbarouk aliwataka watendaji wote kushirikiana kwa karibu na Tume wakati wa utekelezaji wa majukumu yao, ili kupata ufafanuzi au maelekezo pale inapohitajika, na kuhakikisha uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unatekelezwa kwa ufanisi na usahihi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.