SEKTA YA UVUVI
Mkoa wa Pwani una eneo la kilomita za mraba 1,132 lililofunikwa na maji. Sehemu kubwa ya eneo hilo liko kando ya ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi unaoanzia mpaka wa kaskazini wa Wilaya ya Bagamoyo hadi mpaka wa kusini wa Wilaya ya Rufiji. Eneo lote la pwani la Wilaya za Bagamoyo, Mkuranga, Rufiji na Mafia linafaa kwa shughuli za uvuvi. Pa, mito mitatu mikubwa ya Rufiji, Ruvu na Wami inatumika kwa uvuvi.
Uvuvi wa kibiashara
Uvuvi wa kiabishara unaotumia meli za uvuvi hufanyika katika Wilaya zote zilizopakana na Bahari ya Hindi, hata hivyo hakuna meli ya uvuvi iliyosajiliwa Mkoa wa Pwani mpaka sasa. Meli kutoka nje ya nchi na mikoa mingine huvua samaki wengi wanaopatikana katika kina kirefu cha bahari pamoja na kambamiti ambao huchangia sehemu kubwa katika uchumi wa Mkoa na taifa.
Aina ya samaki wanaopatikana
Bahari ya Hindi katika eneo la Mkoa wa Pwani ina aina nyingi za samaki. Samaki wanaopatikana ni pamoja na papa, kasumba panga, dagaa papa, vibua, dagaa mchele, jodari, nguru, sansuli, suli suli, mzira, karambisi, mwatiko, mkundaji (mkisi), Kambamiti, taa, chaza na aina nyingine za samaki wanaohama hama. Aidha, samaki aina ya kambare na sato hufugwa kwenye mabwawa ya kufugia samaki ya maji baridi.
Umuhimu wa Hifadhi ya Bahari katika shughuli za uvuvi
Usimamizi mzuri wa Hifadhi ya Bahari ya Mafia umesababisha kuongezeka kwa upatikanaji wa samaki wengi katika Halmashauri ya Wilaya ya Mafia ikiwa ni eneo la mtawanyiko la samaki kutoka eneo tengefu. Aidha, uhifadhi huo umepelekea kupatikana kwa aina ya samaki ambao hawakuwapo hapo awali kama vile papa potwe (whale shark) ambao wamekuwa kivutio kikubwa cha watalii na kuiweka Halmashauri ya Wilaya ya Mafia na Mkoa wa Pwani katika ramani ya utalii ya dunia.
Uvuvi wa pweza kwa vipindi
Uvuvi wa pweza wa vipindi katika Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti umeleta manufaa makubwa kwa jamii kutokana na upatikanaji wa pweza wakubwa kwa wingi. Pia, siku ya ufunguzi wa miamba imekuwa maarufu na kupelekea kuwepo kwa tamasha ambalo huwakutanisha watu wengi na kutoa fursa kwa biashara ya pweza na samaki wengine.
Ufugaji wa viumbe maji
Shughuli za ufugaji wa samaki kwenye mabwawa zimeongezeka hasa kwenye maji baridi ambapo mpaka mwaka 2025 jumla ya mabwawa 885 ya ufugaji wa samaki yamechimbwa katika Mkoa wa Pwani. Aidha, ufugaji cha jongoo bahari, unenepeshaji wa kaa na kilimo cha mwani katika Halmashauri za Wilaya za Bagamoyo, Mkuranga, Kibiti na Mafia umeongeza fursa za uwekezaji na kuboresha maisha ya jamii.
Uboreshaji wa mazingira ya kuzalia samaki baharini
Ili kuongeza uzalishaji wa samaki baharini, Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Programu ya AFDP inatekeleza mradi wa kuweka mazingira bandia ya samaki baharini ili kuongeza mazalia ya samaki baharini FADs (Fish Aggregatted Devices). FAD nane (8) kati ya kumi (10) zimesakinishwa.
Uvuvi katika bonde la Mto Rufiji
Uvuvi wa msimu wa mvua za masika wa samaki aina ya kambare na perege katika Mto Rufiji na mabwawa (ox-bow lakes) katika bonde la Mto Rufiji umeendelea kuleta manufaa kwa jamii zinazoishi kando ya bonde la mto huo. Mbinu za kisasa za uvuvi na uhifadhi wa kambare zinahitajika ili kuvua kambare na perege kwa wingi na kuwahifadhi ili kuinufaisha jamii katika kipindi cha mwaka mzima.
Ufadhili wa Serikali na taasisi nyingine katika shughuli za uvuvi
Taasisi ya Bahari Maisha kupitia ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) imetoa jumla ya vihori 13 (boti ndogo za kubebea mwani) kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo ambavyo ni vitendea kazi kwa ajili ya shughuli za ukulima wa mwani kwa vikundi 13.
Wizara ya Mifugo na Uvuvi inatekeleza ujenzi wa shamba darasa la ufugaji wa samaki lenye mabwawa manne (4) kwa thamani ya shilingi milioni 169 katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkuranga. Mabwawa hayo yatakabidhiwa kwa kikundi cha ufugaji wa samaki ambapo wananchi wengine watajifunza kupitia wao.
Ili kuongeza tija kwa wavuvi wadogo na wakulima wa zao la mwani, Serikali imetoa mikopo ya boti 39 kwa wavuvi binafsi, vikundi vya wavuvi, makampuni na vyama vya wavuvi katika Mkoa wa Pwani.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.