Afisa elimu Mkoa wa Pwani Sara Mlaki amewataka Maafisa wanaosimamia elimu mkoani humo kuhakikisha wanalinda usalama wa Wanafunzi wawapo shuleni.
Mlaki aliyasema hayo jana Februari 24, 2023 katika kikao kazi cha siku mbili katika shule ya Sekondari Bagamoyo kilichowakutanisha Maafisa toka Idara ya Elimu Msingi, wathibiti ubora elimu, maafisa mipango na maafisa maendeleo ya jamii kutoka halmashauri zote za Mkoa wa Pwani kufanya tathmini ya Utekelezaji wa mpango wa lipa kulingana na matokeo - EP4R wa 2022/2023 na kuandaa mpango wa 2023/2024 katika halmashauri hizo kama sehemu ya matokeo ya Mradi wa Shule Bora kwa ushirikiano na TAMISEMI na Wizara ya Elimu unaofadhiliwa na Serikali ya Uingereza kupitia shirika la misaada la UKAID ukitekelezwa katika mikoa tisa ya Tanzania.
Katika sehemu ya hotuba yake, Mlaki alisisitiza kuwa shule iwe ni sehemu salama kwa mwanafunzi kwani kwa sasa kumekuwa na mmomonyoko wa maadili na ukatili katika jamii na waathirika wakiwa ni watoto.
"Hakikisheni kuwa kwa kushirikiana na jamii, mnalinda usalama wa Wanafunzi wawapo shuleni na nje ya mazingira ya shule, wawe salama kwani Kwa sasa kumekuwa na mmomonyoko wa maadili kwa baadhi ya watu unaosababisha ukatili kwa watoto katika jamii.
Kwa upande wake Mratibu wa lipa kulingana na Matokea (EP4R) Kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Mary Machaku amesema ameona mikakati mizuri inayolenga kuboresha elimu kwa utekelezaji wa mpango huo kutoka kwa washiriki na akawasihi kwenda kuitekeleza ikiwa ni pamoja na utoaji wa chakula shuleni,
kuondoa Changamoto ya KKK (Kusoma, Kuhesabu na Kuandika) na akaongeza kuwa Kwa iwapo washiriki hao watasimami na kutekeleza viashiria walivyoainisha, watafanikiwa kuondoa changamoto zinazoonekana kwenye sekta ya Elimu nchini.
Nao maafisa kutoka halmashauri za Mkoa huo walioshiriki kwenye kikao kazi hicho walieleza kuwa utekelezaji wa mpango wa EP4R umekuwa wa manufaa kwa kuwa umewezesha ongezeko la Ujenzi wa vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo, kisima cha Maji Kibaha ununuzi wa vifaa vya TEHAMA Kwa baadhi ya halmashauri na matumizi ya vitabu huku Mafia wakivuka lengo la uandikishaji wa Watoto wa Awali na Msingi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani
Sanduku la Posta: 30080 Kibaha
Simu ya Mezani: 023 2402287/2402500
Simu ya Mkononi: 023 2402287/2402500
Barua pepe: barua@pwani.go.tz
Hakimiliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani. Haki zote zimehifadhiwa.